• Watoto wachanga wafariki Ghaza kutokana na mzingiro wa kinyama wa Israel

Kituo cha kutetea haki za binadamu Palestina kimetoa taarifa na kusema watoto sita wachanga wameaga dunia katika hospitali za Ukanda wa Ghaza kutokana na mzingiro wa kinyama uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kupelekea hospitali kukosa dawa za dharura.

Taarifa hiyo imesema watoto hao wachanga wameaga dunia kutokana na kukosekana dawa aina ya Surfactant ambayo huwasiadia kupumua watoto waliozaliwa kabla ya wakati.

Nasir Bulbul Mkuu wa Kitengo cha Watoto katika Hospitali ya Shifaa ya Ghaza amesema kila mwezi wanahitaji dawa 100 za Surfacant lakini kutokana na mzingiro uliowekwa na Israel  wanapata dawa 20 tu kila mwezi.

Bulbul ametoa wito kwa Serikali ya Uokozi wa Kitaifa Palestina ichukue hatua za kuokoa watoto wachanga Wapalestina ambao wanazaliwa kabla ya wakati. Aidha ametoa wito kwa jamii ya kimatiafa ichukue hatua za kivitendo kuhitimisha mzingiro wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel uliweka mzingira wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Kiislamu ya Hamas kuongeza eneo hilo. Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani. Misri inashirikiana na Israel katika kuwawekea Wapalestina mzingiro kwani njia ya nchi kavu inayounganisha Ghaza na nchi zingine duniani ni kupitia mipaka ya Misri.

Eneo moja la raia katika Ukanda wa Ghaza lililoharibiwa katika hujuma ya ndege za Israel

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa mbali na miundo mbinu ya eneo hilo kama vile mahospitali, shule na nyumba za raia kuharibiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitahadharisha Jumatatu ya jana kwamba, kwa mujibu wa utafiti wa umoja huo ni kuwa, kufikia mwaka 2020 eneo la Ukanda wa Gaza halitafaa kwa ajili ya kuishi.

Tags

Feb 20, 2018 15:44 UTC
Maoni