• Jeshi la Lebanon: Tutamia nguvu zote kuukabili uvamizi wa Israel

Jeshi la Lebanon limeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuanzisha vita vipya dhidi ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa litatumia mbinu na uwezo wake wote kuzima uvamizi tarajiwa.

Mkuu wa Majeshi ya Lebanon, Jenerali Joseph Aoun ameyasema hayo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Nasisitiza tena kuwa, nchi hii inapinga vikali harakati yoyote ya adui Israel ya kukanyaga haki ya mipaka, kujitawala na kuvumbua rasilimali za kiuchumi za Lebanon."  

Mapema mwezi huu, Rais wa Lebanon Michel Aoun aliliagiza jeshi la nchi hiyo kuwa macho dhidi ya njama zozote za utawala haramu wa Israel za kujaribu kudhalilisha uhuru wa kujitawala nchi hiyo.

Makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Lebanon

Matamshi hayo yametolewa baada ya Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Avidgor Lieberman kutoa vitisho baada ya Lebanon kutangaza zabuni za uchimbaji mafuta na gesi katika eneo la mipaka yake ya Bahari ya Mediterranean.

Kadhalika Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imeutahadharisha utawala haramu wa Israel usithubutu kutoa vitisho kwa Lebanon.

Wanamapambano wa Hizbullah walilisaidia jeshi la Lebanon kupata ushindi dhidi ya chokochoko za Israel dhidi ya nchi hiyo katika vita vya mwaka 2002 na 2006.

Tags

Feb 21, 2018 07:30 UTC
Maoni