• Hamas: Matamshi ya Haley yanadhihirisha uadui wa Marekani dhidi ya Wapalestina

Afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa matamshi yaliyotolewa na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley yamedhihirisha tena uadui wa serikali ya Washington dhidi ya watu wa Palestina.

Sami Abu Zuhri ameyasema hayo kufuatia matamshi ya kuchukiza yaliyotolewa na Haley katika Umoja wa Mataifa kuhusu mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Israel. 

Nikki Haley amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, uamuzi wa kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv kamwe hautabadilishwa hata kama utamkasirisha Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Mwakilishi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliyasema hayo baada ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas kuhutubia Baraza la Usalama akitaka kuanzishwa mchakato mpya wa amani Mashariki ya kati chini ya usimamizi wa kimataifa badala ya Marekani ambayo haiaminiki na inapendelea upande mmoja. 

Abbas alikosoa siasa za Marekani na Uingereza kuhusu kadhia ya Palestina na kusema: Uingereza inahusika katika kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina kutokana na Azimio la Balfor (Balfour Declaration). 

Mahmoud Abbas

Azimio hilo lililotolewa tarehe Pili Novemba mwaka 1917 na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Arthur James Balfour ndilo lililoandaa mazingira ya kuundwa dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina iliyokuwa chini ya ukoloni wa London.

Sami Abu Zuhri amesema baada ya matamshi yasiyo na chembe ya haya ya Nikki Haley kwamba, anatarajia kuwa Mahmoud Abbas ameelewa kwamba mchakato wa mapatano na Wazayuni umefika ukingoni. 

Tags

Feb 21, 2018 14:37 UTC
Maoni