Mar 03, 2018 05:08 UTC
  • Israel: Tumepoteza uwezo wetu mkubwa mbele ya harakati ya Hizbullah na Hamas

Kamanda wa vikosi vya ardhini vya utawala haramu wa lsrael amekiri kwamba, jeshi la utawala huo limepoteza uwezo wake mkubwa mkabala wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Harakati ya muqawama wa Palestina HAMAS.

Cubby Barack, kamanda wa vikosi vya ardhini vya jeshi la lsrael ameongeza kuwa, kwa sasa lsrael imepoteza uwezo mbalimbali mbele ya harakati hizo na kwamba nyenzo za uwezo wa jeshi la Israel za huko nyuma hivi sasa hazipo tena mikononi mwa jeshi hilo.

Benjamin Netanyahu ambaye utawala wake umezingirwa na muqawama

Kabla ya hapo mtandao mmoja wa habari wa Israel ulimnukuu Barack akisema kuwa, hivi sasa harakati ya Kiislamu ya Palestina Hamas ina makombora yasiyopungua elfu 15 katika Ukanda wa Gaza na kwamba vita vijavyo na harakati hiyo vitatofautiana sana na vita vingine vilivyopita. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, kuongezeka uwezo wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah na stratijia mpya inayotumiwa na harakati hiyo, ni mambo ambayo yamezidi kuitia tumbojoto Israel. Wakati huo huo Alex Fishman, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa gazeti la utawala wa Kizayuni la Yedioth Ahronoth amevinukuu vyanzo vya ngazi ya juu vya jeshi la Israel vikielezea wasi wasi wao kutokana na tishio kubwa linaloukabili utawala huo bandia hususan katika uga wa makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Moja ya makombora ya Iran yanayoitia kiwewe Israel na washirika wake

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo makombora yenye uwezo mkubwa ya Iran yanaweza kubadili mlingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba uwezo wote iliyonayo Israel hauwezi kuudhaminia utawala wa Kizayuni usalama wake mbele ya makombora hayo ya Iran. Inafaa kuashiria kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi ya muqawama yamekuwa na nafasi muhimu katika kukabiliana na njama za utawala haramu wa Israel katika eneo.

Tags

Maoni