• Uwongo wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kuhusu Yemen

Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye amefanya safari nchini Misri amesema mbele ya waandishi wa habari wa Misri kuwa vita vinakaribia kumalizika huko Yemen kwa sababu tayari amekwishatimiza malengo yake ya kumuunga mkono rais aliyejiuzulu wa Yemen na ambaye amekuwa akiitambua serikali yake kuwa ni serikali halali.

Bin Salman amedai kuwa na hapa ninamnukuu, "sisi nchini Yemen tunakabiliwa na watu kadhaa tu waliosalia wa harakati ya Ansarullah," mwisho wa kunukuu.

Muhammad bin Salman ametoa madai hayo katika hali ambayo wapiganaji wa harakati ya Ansarullah na pia waitifaki wake kila siku hupata mafanikio makubwa katika oparesheni zake dhidi ya maeneo na ngome za mamluki wa  muungano vamizi wa Saudia; huku utawala huo  ukikaribia kushindwa kikamilifu.  

Viongozi wa Saudia ambao wanajaribu kila njia ili kuhalalisha jinai zao huko Yemen na kuficha kushindwa kwao nchini humo hivi sasa wanahaha bila ya kujua hatima ya uvamizi wao huo huko Yemen. Madai ya uwongo na yasiyo na msingi ya viongozi wa Saudi Arabia yenye lengo la kuficha kushindwa kwa utawala wa Aal Saud katika eneo la Mashariki ya Kati kukiwemo katika vita vilivyoanzisha dhidi ya Yemen, yamekabiliwa na radiamali na misimamo ya wazi dhidi ya utawala huo kidhabu.

Muhammad bin Salman

Kuhusiana na suala hilo, duru za kisiasa zimeyataja madai ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kwamba nchi hiyo imeshinda katika vita huko Yemen kuwa ni njozi tupu. Fikra za waliowengi katika eneo zinaona kuwa ni jambo la mzaha sana kumuona Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia akizungumzia kupata ushindi mkubwa huko Yemen baada kubainika wazi kushindwa vibaya Saudia katika uvamizi wake dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Matukio ya Yemen yanaonyesha kuwa  madai ya uwongo na upotoshaji yanayotolewa na viongozi wa Saudia hayawezi kuficha kushindwa kwake katika eneo hili la Mashariki ya Kati. 

Sameh Askar mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Misri amesema katika mahojiano na gazeti la al Watan kuwa: Utawala wa Aal Saud umefeli katika vita dhidi ya wananchi waliodhulimika wa Yemen kwa upande wa kisiasa, kijeshi na kiakhlaqi. Abdulsattar Qassim ameandika makala kwenye gazeti la al Rai al Youm kuwa: Kwa siasa zake hizo Saudia imedhihirisha kuwa ni nchi inayopenda vita na kuzusha migogoro na sasa imekwama katika kinamasi ilichojisababishia yenyewe. 

Madai ya viongozi wa Saudi Arabia ya kuhalalisha uingiliaji wa nchi hiyo huko Yemen yanatolewa katika hali ambayo natija ya uingiliaji kati huo na uvamizi wa kijeshi wa Riyadh huko Yemen ni kuuliwa raia wengi wa nchi hiyo, kuharibiwa miundo mbinu na kuisababishia nchi hiyo maafa na hasara chungu nzima. Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi ya anga na makombora  huko Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa baraka za Marekani.

Mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen, raia wauliwa na nyumba kubomolewa

Hii ni katika hali ambayo baada ya kupita karibu miaka mitatu tangu kuanza vita huko Yemen na kutekelezwa mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia nchini humo;  Saudia na nchi nyingine waitifaki wake katika vita hivyo hivi sasa zinajaribu kuhitimisha vita hivyo au kwa maneno mengine, zinataka kujitoa kwa heshima katika hali hiyo bila ya mafanikio yoyote. Saudia ambayo ilianzisha vita dhidi ya Yemen ilitaraji kwamba vita hivyo vingemalizika haraka sambamba na kutoa pigo kwa harakati ya Ansarullah na hivyo kufanikiwa kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansour Hadi Rais mstaafu wa Yemen ambaye ni kibaraka wa nchi za Magharibi ina Saudi Arabia. Hata hivyo vita hivyo vimeshindwa kumalizika katika muda mfupi na vingali vinaendelea. Sababu kuu ni kuwa utawala wa Saudia ulipuuza nguvu ya muqawama wa wananchi wa Yemen. Hii ni katika hali ambayo kufanyika maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Yemen dhidi ya muungano vamizi wa Saudi Arabia na kushiriki matabaka tofauti ya Wayemeni kwenye maandamano hayo; ni sawa na kudhihirishwa wazi hasira za wananchi wanamapinduzi wa Yemen kwa utawala wa Aal Saud  na sisitizo lao la kuupinga utawala wa Saudi Arabia, jambo ambalo bila shaka ni dhihirisho la wazi la kushindwa Aal Saud katika medani ya vita huko Yemen.   

Abdu Rabbuh Mansour Hadi, Rais aliyejiuzulu wa Yemen 

Tags

Mar 07, 2018 08:01 UTC
Maoni