• Hizbullah: Saudia na Marekani zinaingilia uchaguzi wa Lebanon

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa Saudi Arabia na Marekani zinakula njama ya kuingilia uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo unaotazamiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Sheikh Naim Qassim ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Manar na kuongeza kuwa, Riyadh na Washington zinafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa idadi ya wawakilishi wa haharakati hiyo katika Bunge la Lebanon inapungua kwa kiasi kikubwa.

Amewataka wananchi wa Lebanon kutopigia kura wanasiasa ambao wapo tayari kuiuza na kuikabidhi nchi yao kwa Marekani na Saudia kwa madhara ya uchumi na rasilimali za nchi hiyo.

Februari 28, Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri alielekea mjini Riyadh, Saudi Arabia kufuatia mwaliko wa mjumbe maalumu wa Mfalme Salman wa nchi hiyo, ikiwa ni safari ya kwanza kufanywa naye tangu alipotangaza kujiuzulu uwaziri mkuu wa Lebanon tarehe 4 Novemba 2017 akiwa katika mji mkuu huo wa Saudia.

Saad Hariri na Mfalme wa Saudia mjini Riyadh

Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah aliwatahadharisha wananchi wa Lebanon wasije wakanasa kwenye mtego wa maadui zao, akiweka bayana kuwa Marekani inataka kushirikiana na Israel kuvuruga uthabiti wa nchi hiyo, kwa lengo la kuvamia na kufyonza visima vya mafuta vya nchi hiyo ya Kiarabu.

Alisema Walebanon kuiunga mkono Hizbullah katika uchaguzi ujao, ni kulinda damu za mashahidi ambao walitoa muhanga roho zao kwa ajili ya harakati ya muqawama. Uchaguzi wa Bunge wa Lebanon umepangwa kufanyika Mei 6 mwaka huu. 

Tags

Mar 08, 2018 16:03 UTC
Maoni