Mar 10, 2018 07:48 UTC
  • Syria: Madai ya Marekani dhidi yetu yanalenga kuwapa himaya magaidi

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema tuhuma zilizotolewa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya Damascus hazina madhumuni mengine ghairi ya kuyakingia kifua na kuyapa himaya makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Bashar Ja'afari ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la Russia na kuongeza kuwa, waungaji mkono wa magenge ya kigaidi nchini Syria wametoa matamshi ya uwongo na yasiyo na msingi ili kuyashajiisha na kuyapa moyo makundi hayo ya kigaidi yanayoeleka kusambaratika kikamilifu.

Amesema tuhuma hizo za Marekani kwamba serikali ya Damascus ilitumia silaha za kemikali eneo la Ghouta Mashariki zinalenga kuongeza mashinikizo ya kusalimu amri serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.

Sehemu ya silaha za US zilizopatikana mikononi mwa magaidi Ghouta Mashariki

Madai hayo ya Washington na waitifaki wake yanatolewa katika hali ambayo, jeshi la Syria Alkhamisi ya juzi lilikamata kiwango kikubwa cha silaha na zana za kijeshi pamoja na mada za miripuko zilizotengenezwa nchini Marekani, katika maficho ya magaidi huko Ghouta Mashariki, viungani mwa mji mkuu, Damascus.

Syria ilitumbukizwa kwenye mgogoro mkubwa mwaka 2011 baada ya nchi za Magharibi kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za eneo hasa Saudi Arabia, kumimina magaidi kutoka kila kona ya dunia ndani ya ardhi ya Syria, na kuwapa silaha na mafunzo ya kijeshi ili wavuruge amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu, na kuandaa uwanja wa kumng'oa madarakani rais halali wa nchi hiyo.

Tags

Maoni