Mar 14, 2018 03:35 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon: Quds itabakia milele kuwa mji mkuu wa Palestina

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa njia ya ufumbuzi wa kadhia ya Palestina haiko mikononi mwa Marekani, bali kinachopasa kufanywa ni kuzifuatilia jinai zinazotendwa na Marekani.

Sheikh Naim Qassem aliyasema hayo hapo jana katika mkutano wa nne wa kimataifa wa kuonyesha mshikamano na Palestina unaofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kubainisha kwamba maamuzi yanayopitishwa na Marekani hayana umuhimu, kwani Baitul Muqaddas itabakia milele kuwa mji mkuu wa Palestina na muqawama wa mtutu wa bunduki ndio njia ya kwanza ya kuikomboa Palestina.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa wale viongozi wa Waarabu wanaotaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel hawana haki ya kuwa watawala wa mataifa yao.

Mandhari ya mji wa Baitul Muqaddas, ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu 

Sheikh Muhammad Hussein, Mufti wa Quds tukufu, ambaye naye pia amehutubia mkutano huo amesema, Baitul Muqaddas inakabiliwa na hujuma mbaya kabisa za Wazayuni na kwamba maghasibu wa Kizayuni wanafanya njama za kufuta ustaarabu na athari za Kiarabu na Kiislamu katika ardhi za Palestina kupitia utungaji wa sheria mpya.

Mufti wa Quds ameashiria uamuzi uliotangazwa tarehe 6 Desemba mwaka jana na Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kueleza kwamba hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa na kaununi za kibinadamu.

Mkutano wa nne wa kimataifa wa kuonyesha mshikamano na Palestina unaohudhuriwa na shakhsia wa Kipalestina na wale wenye kuihami Quds tukufu ulianza siku ya Jumapili ya tarehe 11 Machi mjini Beirut, Lebanon na unatazamiwa kumalizika rasmi hii leo.../

Tags

Maoni