Mar 20, 2018 07:38 UTC
  • Mbali na Uturuki kuivamia Syria, Erdoğan atishia tena kuishambulia Iraq

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametishia kwamba, ikiwa serikali ya Iraq haitoshirikiana na nchi yake, basi Ankara itaanzisha mashambulizi katika miji ya Sinjar nchini Iraq dhidi ya wanachama wa kundi la Kikurdi la PKK.

Erdoğan aliyasema hayo jana Jumatatu mjini Istanbul na kuongeza kuwa, kwa mara kadhaa Uturuki imeifahamisha serikali kuu ya Iraq kwamba, miinuko ya eneo la Sinjar iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu, imegeuka kuwa eneo la kukusanyikia wale aliowaita kuwa ni magaidi na kwamba iwapo serikali ya Baghdad haitowasambaratisha, basi Uturuki itafanya mashambulizi hayo yenyewe.

Jeshi la Uturuki lilipovamia maeneo ya kaskazini mwa Iraq miaka michache iliyopita

Kadhalika rais huyo wa Uturuki amedai kwamba milima hiyo ya Sinjar iliyoko umbali wa kilomita 100 katika mpaka wa Uturuki na karibu na mpaka wa Syria pamja na miinuko ya Qandil ya Iraq iliyoko karibu na mipaka ya Iran, ni ngome za wapiganaji wa Kikurdi wa PKK. Serikali ya Uturuki inalitambua kundi la PKK kuwa ni la kigaidi na tangu mwaka uliopita wa 2017, ilianzisha operesheni kubwa ndani ya ardhi ya Uturuki na hata kaskazini mwa Iraq kwa kile kilichotajwa na serikali ya Ankara kuwa ni kwa ajili ya kuwaangamiza wapiganaji wa kundi hilo. Mchakato wa kutatuliwa tatizo la Wakurdi nchini Uturuki, ulianza mwezi Disemba mwaka 2012, hata hivyo mchakato huo ulisimama baada ya kutokea mripuko wa mwaka 2015 mjini Suruç Uturuki. Kuanzia wakati huo, jeshi la Uturuki lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya wanachama wa kundi hilo.

Wapiganaji wa Kikurdi wa PKK ambao wanapambana na jeshi la Uturuki

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, katika kipindi hicho kwa akali askari 600 wa Uturuki na zaidi ya wanachama 7000 wa kundi la PKK wameshauawa katika makabiliano ya silaha. Aidha Uturuki imetangaza kwamba, hakuna tena njia ya utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Wakurdi nchini humo na kwamba matukio ya hivi karibuni yamepoteza nafasi ya mwisho ya utatuzi wa kidiplomasia wa kadhia ya kundi la PKK. Hii ni katika hali ambayo shakhsia mbalimbali wa kisiasa nchini Uturuki wamekuwa wakikosoa siasa za Rais Recep Tayyip Erdoğan za kupenda vita badala ya kutumia njia za amani, na kwamba siasa hizo zitaigharimu pakubwa Uturuki hapo baadaye.

Tags

Maoni