Mar 20, 2018 07:54 UTC
  • Marekani yakasirika baada ya balozi wake Israel kuitwa mbwa na Mahmoud Abbas

Ikulu ya Marekani White House imekasirishwa sana na matamshi ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kumwita balozi wa Marekani mjini Tel Aviv kuwa ni mwana wa mbwa.

Jana Jumatatu Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akizungumza mjini Ramallah, alimtaja David Melech Friedman, balozi wa Marekani mjini Tel Aviv, kuwa ni mwana wa mbwa kutokana na hatua ya balozi huyo kuunga mkono ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Kufuatia hatua hiyo, White House imelaani vikali na kusema kuwa, matamshi hayo ya Abbas ni ya kudhalilisha.

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Katika matamshi yake Mahmoud Abbas alisema kuwa, rais wa Marekani Donald Trump anautambua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina kuwa ni wa kisheria huku viongozi wengi wa ngazi ya juu wa Marekani akiwemo pia David Friedman, balozi wa Marekani mjini Tel Aviv wakiwa wanakariri madai hayo ya Trump kwamba eti Wazayuni wanajenga katika ardhi zao. Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kwamba, balozi huyo wa Marekani huko Israel ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kama ambavyo pia ni muungaji mkono mkuu wa maamuzi ya Trump ya kuitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala khabithi wa Israel na suala la kuhamishiwa Quds ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv.

David Melech Friedman balozi huyo wa Marekani mjini Tel Aviv aliyetajwa na Abbas kuwa ni mbwa

Trump aliutangaza mji wa Quds (Jerusalem) ambao unaheshimiwa na Waislamu na Wakristo na Mayahudi, kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel mwezi Disemba mwaka jana, na kutaka kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda mjini humo, suala ambalo linaendelea kulaani hadi leo hii duniani.

Maoni