Apr 19, 2018 03:03 UTC
  • Magaidi elfu tano (5000) walazimika kuondoka katika viunga vya mji mkuu wa Syria

Hatimaye, genge la kigaidi la Jeish al Islam limetangaza kuwa limekubali kuondoa wanamgambo wake 5,000 waliko katika eneo la al Dhamir katika viunga vya mji mkuu wa Syria Damascus na kuwapelekea Jarabulus mkoani Halab (Aleppo) pamoja na familia zao.

Shirika la habari la Syria SANA limesema kuwa, magaidi wa Jeish al Islam wamelazimika pia kukabidhi silaha zao nzito wa kijeshi na baadhi ya silaha nyepesi kwa jeshi la Syria kama njia ya kuonesha kuwa wako tayari kuondoka katika eneo la al Dhamir, nje ya mji mkuu, Damascus. Hayo yamekuja baada ya magaidi hao kuzidiwa nguvu na jeshi la Syria.

Uamuzi wa kutoa magaidi hao katika eneo la al Dhamir umekuja baada ya magaidi hao kufurushwa katika mji wa Douma huko Ghouta Mashariki na hatimae jeshi la Syria kutangaza kulikomboa rasmi eneo hilo muhimu la kiistratijia Jumamosi usiku.

Ugomvi baina ya magenge mawili ya kigaidi ya Jeysh al Islam na Jabhat al Nusra nchini Syria

 

Habari nyingine kutokana nchini Syria inasema kuwa, jeshi la Russia limegundua ghala moja ililojaa mada za kuzalisha silaha za kemikali katika mji wa Douma. Ghala hilo ni mali ya magaidi waliokuwa wanaudhibiti mji huo.

Igor Nikolin, mmoja wa wataalamu wa kijeshi wa Russia ameliambia shirika la habari la Sputnik kwamba zana hizo zimepatikana katika maabara yaliyokuwa na kinu cha kutengeneza mada za kemikali kilichotengenezwa katika moja ya nchi za Magharibi imma Uingereza au Ujerumani. Maabara hayo yalikuwa yanatumiwa na magenge ya kigaidi kutengeneza mada za sumu.

Ikumbukwe kuwa, Jumamosi alfajiri, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilishambulia maeneo kadhaa ya Syria kwa madai kuwa serikali imetumia silaha za kemikali huko Ghouta Mashariki madai ambayo zimeshindwa kuyathibitisha hadi leo hii.

Tags

Maoni