Apr 19, 2018 07:43 UTC
  • Nyaraka za maktaba ya taifa Qatar zafichua utegemezi aliokuwa nao mwasisi wa Saudia kwa UK

Tovuti ya maktaba ya taifa ya Qatar imeonyesha nyaraka ilizopokea kutoka maktaba ya Uingereza zinazofichua kuhusu utegemezi aliokuwa nao Abdulaziz Aal Saud, mwasisi wa utawala wa Saudi Arabia kwa dola la kikoloni la Uingereza.

Taarifa zilizopatikana katika maktaba ya taifa ya Qatar iliyofunguliwa hivi karibuni na Amir wa nchi hiyo Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, mbali na kubainisha maandikiano, ripoti za kiidara, hati za maelewano na maandiko ya mkono ya mwasisi wa utawala wa Aal Saud, zinajumuisha pia maandikiano yaliyokuwepo kati ya Abdulaziz Aal Saud na idara za kisiasa za Uingereza katika nchi za Bahrain, Kuwait, Jeddah, mwakilishi wa juu katika nchi za Iraq na Misri, Idara ya Uingereza India na wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

Ofisi ya ufalme wa Saudi Arabia imethibitisha kupitia ukurasa wake rasmi wa twitter usahihi wa nyaraka hizo ambazo zimetolewa pia na Abdullah al Adhba, mhariri wa gazeti la Al-Arab linalochapishwa nchini Qatar.

Barua ya Mfalme Abdulaziz ya kuipa hakikisho Uingereza la kuafiki kuundwa utawala wa kizayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina

Abdulaziz bin Saud, aliyejulikana kama Mfalme Abdulaziz au Ibn Saud ni mfalme wa mwanzo na mwanzilishi wa ufalme wa Saudi Arabia.

Wakati huohuo, Uingereza, ambayo inajiandaa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya inaendelea kufunga mikataba ya kibiashara na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudia ili kuweza kutumia fursa za uwekezaji katika nchi hizo.

Tangu ulipoanza uvamizi na hujuma za kijeshi za Saudi Arabia dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015, serikali ya Uingereza imetoa kibali cha kuiuzia Saudia silaha zinazogharimu zaidi ya pauni bilioni tatu.

Mikataba hiyo inajumuisha mauzo ya ndege za kivita na ndege zisizo na rubani za droni zenye thamani ya pauni bilioni mbili na milioni 200, makombora na mabomu yenye thamani ya pauni bilioni moja na milioni 100 pamoja na magari ya deraya na vifaru vyenye thamani ya pauni laki nne na thelathini elfu.../

 

Tags

Maoni