• Russia: Makundi ya kigaidi Syria yanawazuia wakaguzi wa OPCW kuingia Douma

Nabu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za kigeni huko Syria yanawazuia wakaguzi wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) kuingia katika mji wa Douma ulioko katika viunga ya mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus.

Mikhail Bogdanov ametahadharisha kuwa, magaidi wa eneo hilo la Douma wangali hatari kubwa kwa raia na wataalamu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali.

Amesema kuwa magaidi hao wanawatisha raia na kuingilia kazi za wawakilishi wa jamii ya kimataifa, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wakaguzi wa shirika la OPCW. Ameongeza kuwa kuna pande ambazo hazitaki kufanyike uchunguzi usiopendelea upande wowote kuhusu madai ya utumiaji wa silaha za kemikali katika eneo la Douma.

Douma, Ghouta Mashariki

Wakaguzi wa shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) wameelekea Syria kwa ajili ya kuchunguza maeneo kunakodaiwa kwamba kulitumiwa silaha za kemikali tarehe 7 Aprili.

Madai hayo yalitumiwa na nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa kama kisingizio cha kushambulia maeneo kadhaa na vituo vya utafiti ndani ya nchi ya Syria kabla hata ya kufanyika uchunguzi wa aina yoyote kuhusu madai hayo. Mashambulizi hayo pia yalifanyika bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.   

Tags

Apr 19, 2018 14:27 UTC
Maoni