Mei 10, 2018 02:26 UTC
  • Makombora ya Yemen yaulenga mji mkuu wa Saudia, Riyadh

Wanajeshi wa Yemen wametumia makombora yaliyoundwa nchini humo kushambulia maeneo kadhaa ya kijeshi na kiuchumi ya Saudia Arabia ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh.

Kwa mujibu wa taarifa katika mashambulizi hayo ya Jumatano ambayo ni sehemu ya oparesheni za kulipiza kisasi, Kitengo cha Makombora cha Jeshi la Yemen kimetangaza kuvurumisha makombora yaliyolenga mji mkuu Riyadh na eneo la Najran. Kwa mujibu wa taarifa makombora ya  balistiki y Burkan H2  ya Jeshi la Yemen yamelenga maeneo ya kiuchumi katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh. Aidha makombora mengine aina ya Badr 1 yalivurumishwa kwa mafanikio katika kituo cha Jeshi la Saudia cha Ulinzi wa Anga katika eneo la Jizan. Mashirika ya habari ya kimataifa yameripoti kusikika milipuko ya makombora katika mji wa Riyadh siku ya Jumatano.

Makombora ya Balistiki yaliyotengenezwa nchini Yemen ya Burkan 2

Mashambulizi hayo yote ni katika oparesheni za kulipiza kisasi jinai za Saudia dhidi ya raia wa Yemen. Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh. 

Raia zaidi ya elfu 14  wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi. Aidha watu karibu milioni moja wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote nchini Yemen huku wengine karibu 3,000 wakifariki dunia tokea mwezi Aprili mwaka jana. Mamilioni ya Wayemen pia wamepoteza makazi yao kutokana na hujuma hizo za Saudia.

Tags

Maoni