Mei 22, 2018 14:23 UTC
  • Answarullah: Kuna mpasuko mkubwa katika muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen

Mwakilishi wa Harakati ya Kiislamu ya Answarullah huko Iraq, ameelezea kuwepo mpasuko mkubwa ndani ya safu ya muungano vamizi dhidi ya Yemen ambao unaongozwa na Saudi Arabia.

Mohammed Ahmed Al-Qabli ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA juu ya sababu za kuongezeka tofauti kubwa katika muungano huo na kusema kuwa tofauti hizo zinasababishwa na masuala ya kifedha na tamaa za baadhi ya wanachama wa muungano tajwa. Al-Qabli amesema kuwa, wakati Wasudan ambo ni sehemu ya muungano huo walipogundua kwamba ushiriki wao katika vita nchini Yemen hauna maslahi yoyote ya kifedha, wameamua kujiondoa katika muungano huo vamizi.

Bendera za baadhi ya nchi zinazoishambulia kijeshi Yemen

Ameongeza kwamba tofauti za muda mrefu kati ya Qatar na Saudia zimeipelekea serikali ya Doha kujiondoa katika muungano huo, huku tofauti mpya za hivi karibuni kuhusiana na kisiwa cha Socotra cha Yemen nazo zikishtadi kati ya Wayemen vibaraka na Imarati kwa upande mmoja na Saudia kwa upande wa pili. Mwakilishi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Answarullah huko Iraq amesisitiza kwamba licha ya kuwa hivi sasa njama zinazofanywa dhidi ya Yemen ni kubwa lakini pamoja na hayo taifa la Yemen na jeshi la nchi hiyo limeweza kutoa pigo kubwa kwa wavamizi. 

Tags

Maoni