Mei 23, 2018 03:46 UTC
  • Mwanamfalme wa Saudia ataka kupinduliwa Mfalme Salman

Mwanamfalme mmoja wa Saudi Arabia amewataka wajomba zake wenye ushawishi mkubwa ndani ya utawala wa Aal-Saud kufanya jitihada za kuondolewa madarakani Mfalme Salman bin Abdulaziz ili kuzuia watawala wa sasa wanaongozwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman kuvuruga zaidi mambo na kuupaka matope utawala huo wa kiukoo.

Khaled bin Farhan ambaye Ujerumani ilikubali kumpa hifadhi amewataka wajomba zake Wanawafalme Ahmed bin Abdulaziz na Muqrin bin Abdulaziz kuongoza harakati hizo za kumpindua madarakani Mfalme Salman.

Amewataka wajomba zake hao kutumia ushawishi wao kuwarai wanawafalme wenzao pamoja na jeshi la nchi hiyo ili wamuondoe madarakani Mfalme Salman wa Saudia, kwa lengo la kuzuia uwezekano wa kusambaratika utawala huo wa kifalme.

Amesema, "Mabadiliko hayo ya uongozi ndiyo tu yatakayoukomboa ufamle wa Saudia kutokana na maamuzi ya kipumbavu, ghalati na yasio na mantiki ya Salman."

Khaled bin Farhan, mwanamfalme wa Saudia aliyekimbilia usalama wake Ujerumani

Bin Farhan ameongeza kuwa, "Tayari nimepokea baruapepe nyingi kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu wa polisi na jeshi, wanaounga mkono mwito wangu wa kufanyika mapinduzi Saudia."

Muhammad bin Salman aliteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Juni mwaka jana baada ya safari ya Donald Trump huko Saudia, na wanawafalme wengine wamekuwa wakikosoa vikali sera zake za ndani na nje ya nchi.

Maoni