Mei 23, 2018 06:15 UTC
  • Kurejeshwa usalama kamili Damascus na katika viunga vyake; mafanikio mengine ya Syria dhidi ya magaidi

Kamandi Kuu ya jeshi na vikosi vya ulinzi vya Syria imetangaza kuwa baada ya kufurushwa magaidi wote katika eneo la Hajarul-Aswad na kwenye kambi ya Yarmuk, amani na usalama kamili umerejea katika mji mkuu wa nchi hiyo Damascus na vitongoji vyake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi la Syria limelidhibiti kikamilifu eneo la Hajarul-Aswad na kambi ya Yarmuk; na kabla yake lilividhibiti viunga vitatu vya Yalda, Rabila na Bait Sahm. Taarifa hiyo imefafanua kwamba vitongoji vyote vya Ghouta Mashariki na Magharibi vimeshadhibitiwa kwa kutokomezwa kikamilifu magaidi wa kitakfiri.

Katika miezi ya karibuni, jeshi la Syria limeanzisha operesheni ya kuhitimisha uwepo wa makundi ya kigaidi katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Kuwepo makundi ya kigaidi katika viunga vya Damascus kuliwapa magaidi hao fursa ya kuendeleza ndoto yao ya kuuteka mji mkuu huo wa Syria na Ikulu ya rais wa nchi hiyo. Kwa ujumla kusafishwa kikamilifu maeneo ya vitongoji vya Damascus kwa kufurushwa magaidi wote kwenye maeneo hayo kutafungua zaidi njia kwa ajili ya kusonga mbele jeshi la Syria katika sehemu za kusini na kaskazini magharibi zilizokuwa zikidhibitiwa na magaidi kuliko hata hali ilivyokuwa ulipokombolewa mji wa Aleppo kutoka mikononi mwa magaidi hao; na kwa njia hiyo kuharakisha zaidi operesheni za kuisafisha Syria kwa kuwatokomeza magaidi wote. 

Askari wa jeshi la Syria baada ya kukomboa moja ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa magaidi

Kwa kuzingatia ushindi liliopata jeshi la Syria na waitifaki wake dhidi ya makundi ya kigaidi mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, kwa wiki kadhaa sasa operesheni za mashambulio zimeelekezwa kwenye njia za kuingilia mji mkuu, yaani maeneo ya viunga vya Damascus ili kuyasafisha kwa kutokomeza uchafu wa magaidi uliokuwa umesambaa kwenye maeneo hayo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana makundi ya kigaidi na ukufurishaji yanayoungwa mkono na mhimili wa Magharibi na Waarabu yamejizatiti kuhakikisha yanaendelea kuyadhibiti maeneo hayo ya kistratejia ili yapate njia ya kujipenyeza katika mji mkuu huo wa Syria. Na ndio kusema kuwa kukombolewa maeneo mbalimbali ya viunga vya Damascus kutoka mikononi mwa magaidi ni sawa na kuporomoka ngome ya mwisho ya magaidi na kutoweka ndoto waliyokuwa nayo ya kuudhibiti mji mkuu huo.

Magaidi wa kundi la Tahriru-Sham (Jabhatu-Nusra)

Kuwepo kwa miaka kadhaa makundi ya kigaidi ya mataifa mbalimbali katika maeneo hayo, ambayo kila moja ni kibaraka na mamluki wa moja kati ya nchi za mhimili wa Magharibi na Waarabu, kumekuwa muda wote kukitumiwa na nchi hizo kama wenzo wa kujiweka karibu na kitovu cha mhimili wa kisiasa wa Syria na karata yao ya turufu ya kupatia fursa na kutoa mashinikizo kwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo. Na ni kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa eneo hilo, ndio maana hatua ya jeshi la Syria ya kuyakomboa na kuyasafisha maeneo ya kandokando mwa Damasacus imezidi kuwatia tafrani na kuwaghadhibisha waungaji mkono wa magaidi. Matukio yanayojiri kwenye medani za vita nchini Syria yanaashiria vipigo vikali ambavyo magaidi wanaendelea kuvipata kutoka kwa jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo.

Kutokana na matukio na mabadiliko yanayojiri nchini Syria, inavyoonekana, saa za kutokomezwa na kutoweka ugaidi katika ardhi ya nchi hiyo zimeanza kuhesabika. Kituo cha habari cha Sputnik, hivi karibuni kilichapisha makala iliyoandikwa na Nawaf Ibrahim inayoeleza kwamba, kwa msaada na uungaji mkono wa kambi ya muqawama, serikali ya Syria imeweza kuwarejeshea waungaji mkono wa ugaidi njama yao; na ndoto waliyokuwa nayo ya kuiangusha serikali ya Syria na kuigawanya nchi hiyo vipande vipande haikufikiwa.

Rais Bashar al-Assad wa Syria akiwaamkia wananchi

Matukio ya Syria yanaonyesha mabadiliko yanayozidi kujiri katika mlingano wa nguvu kwenye uga wa uchukuaji hatua na katika medani za mapambano kwa manufaa ya mfumo wa wananchi unaotawala nchi hiyo, sambamba na mafanikio linayozidi kupata jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi hao. Kushindwa magaidi katika vitongoji vya mji wa Damascus ni nukta nyingine muhimu sana katika muqawama wa wananchi wa Syria ambayo matunda na athari zake hazijaishia kwenye uga wa medani za vita tu bali zimeonekana pia katika uga wa kisiasa na kimataifa. Miongoni mwa matunda hayo ni kuzidi kujizatiti na kuwa imara zaidi nafasi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.../

Tags

Maoni