• Berri achaguliwa tena kuwa Spika wa Bunge la Lebanon, ataka dunia iizuie Israel

Nabih Berri amechaguliwa tena kuwa Spika wa Bunge la Lebanon ambalo limekutana leo baada ya uchaguzi uliofanyika Mei 6.

Berri amefanikiwa kupata kura 98  katika bunge hilo lenye viti 128 na hivyo kumuwezesha kuendelea kuwa spika wa bunge hilo kwa muhula wa sita sasa tokea mwaka 1992.

Akizungumza punde baada ya kuchaguliwa, Berri amewashukuru wananchi wa Lebanon kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa bunge. Amesema katika miaka ya hivi karibuni magaidi walikuwa wanalenga maeneo ya mpaka wa masahriki na kaskazini mwa Lebanon na kwamba bunge limekuwa pamoja na wananchi katika kuliunga mkono jeshi.

Bunge la Lebanon

Aidha amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kuwa tishio kwa usalama na amani duniani.

Nabih Berri pia amesisitiza kuhusu kuuendelea kuwaunga mkono wa Palestina na haki yao ya kurejea katika ardhi zao za jadi sambamba na kuundwa taifa huru la Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem).

Berri hakuwa na mpizani katika kuwania kiti cha uspika wa bunge ambacho kwa mujibu wa mpango wa kugawana madaraka Lebanon kinapaswa kushikiliwa na Mwislamu wa madhehebu ya Shia nayo nafasi ya waziri mkuu ni lazima ishikiliwe na Mwislamu wa madhehebu ya Sunni na rais wa nchi naye anatakuwa kuwa Mkristo wa Kimaronite.

Mei 23, 2018 14:19 UTC
Maoni