Mei 25, 2018 03:17 UTC
  • Msikiti wa al Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu
    Msikiti wa al Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, vitendo vya balozi wa Marekani vinaonesha jinsi nchi yake inavyoshirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuyavunjia heshima matukufu ya taifa la Palestina na ya umma mzima wa Kiarabu na wa Kiislamu.

Hivi karibuni kumesambazwa picha ya David Friedman, balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu inayoonesha Msikiti wa al Aqsa na Quba al Sakhra vimevunjwa na mahala pake pana hekalu la Kizayuni. Aidha na ikiwa ni katika kuendeleza njama na uadui wa Marekani dhidi ya Quds katika kipindi cha urais wa Donald Trump huko Marekani, hivi karibuni utawala wa Kizayuni ulichukua hatua ya kichokozi ya kutengeneza modeli ya Hekalu la Kizayuni na kuliweka mkabala wa Masjid al Aqswa ambacho ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. 

 

Wazayuni wanaendelea kukaidi maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria zote za kimataifa kutokana na uungaji mkono wa Marekani, na daima wanafanya njama za kufuta kikamilifu utambulisho wa Kiislamu na kihistoria wa taifa la Plestina na mahala pake kuweka nembo bandia za Kizayuni. Hayo yanatendeka katika hali ambayo Marekani haikutosheka na kutoa baraka tu kwa viongozi wa utawala wa Kizayuni ya kuendeleza siasa zao za kijuba na uharifibu wao huko Baytul Muqaddas, bali mara kwa mara viongozi wa Marekani wamekuwa wakishiriki moja kwa moja katika harakati za mirengo yenye misimamo mikali ya Kizayuni dhidi ya Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa na kuzidi kuwachochea na kuwatia nguvu Wazayuni ya kuendeleza jinai zao dhidi ya Wapalestina.

Miaka kadhaa iliyopita, Bill Johnson na David McNally wabunge wa zamani wa Marekani walifuatana na magenge yenye misimamo mikali ya Kizayuni kuuvamia Msikiti wa al Aqsa. Kiujumla ni kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni zinafanya njama hatari sana za kujaribu kudhibiti kila kitu huko Baytul Muqaddas kama njia ya kuendeleza uharibifu wao dhidi ya matukufu ya Kiislamu. Jambo hilo kwa kweli linazidi kuonesha malengo ya nyuma ya pazia ya Marekani. Miongoni mwa njama hizo ni kile kinachodaiwa kuwa ni "Mapatano ya Karne" ambapo inasikitisha kuona kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Saudi Arabia zinashiriki kwenye njama hizo za Marekani.

Bendera iliyochanikachina ya Israel

 

Hatua za hivi sasa za Marekani zinaonesha kuanza kipindi kipya cha njama za kuuharibu Msikiti wa al Aqsa. Itakumbukwa kuwa, kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Mapatano ya Karne" mji mtakatifu wa Quds lazima ukabidhiwe kikamilifu mikononi mwa utawala wa Kizayuni wa Israel na pia zifutwe athari na maeneo yote ya Kiislamu na kuyapa sura ya Kizayuni. 

Najih Bakirat, mkuu wa hivi sasa wa masuala ya kisheria na wakfu wa Kiislamu ya Quds amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni unatumia fursa ya hatua ya Marekani kuuhamishia Quds ubalozi wake kutoka Tel Aviv kama kificho cha kutekelezea siasa zake za uharibifu. Israel inataka kufuta kabisa utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa Quds na kuangamiza taasisi zote za Wapalestina katika mji huo mtakatifu. Hata hivyo na licha ya kuweko njama zote hizo, lakini Wapalestina wataendelea kuwepo katika mji wa Quds na Masjid al Aqswa kama ambavyo pia wataendelea kupambana na njama zote kwa uwezo na nguvu zao zote.

Matukio ya Palestina nayo yanathibitisha kuwa njama za Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao zitafeli tu hasa katika kipindi hiki cha kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Maandamano ya Wapalestina yanaendelea, njama za Marekani za "Mapatano ya Karne" zimepingwa vikali na Wapalestina wa mirengo yote na kadiri siku zinavyopita ndivyo Intifadha ya Wapalestina inavyozidi kupata nguvu. Pamoja na hayo yote, inabidi pia Wapalestina na ulimwengu mzima wa Kiislamu uzidi kuwa macho mbele ya njama za kiuadui za Marekani, Israel na vitimbakwiri vyao.

Tags

Maoni