Mei 26, 2018 07:43 UTC
  • IMF: Marekani iangalie upya sera zake dhidi ya Iran na Russia

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani IMF amemuasa Rais Donald Trump wa Marekani kuangalia upya sera zake za kushadidisha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia.

Christine Lagarde alitoa mwito huo jana Ijumaa alipokuwa akihutubu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa St. Petersburg nchini Russia na kuongeza kuwa, Marekani inapaswa kuangalia upya sera hizo haswa kwa kuzingatia kuwa malengo ya sera zenyewe hayaeleweki.

Mkuu huyo wa IMF amesema sera ngumu za kifedha za Marekani, na kuziwekea vingiti baadhi ya nchi katika mabadilishano ya bidhaa na huduma, ni katika mambo yanayoupa changamoto mfumo wa kiuchumi duniani.

Mei 8 Trump alitangaza kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo serikali iliyotangulia ya Marekani ilikuwa imeyaidhinisha.

Trump baada ya kuindoa Marekani katika JCPOA

Huku akikariri matamshi yasiyo na msingi ya chuki dhidi ya Iran, Trump alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.

Jamhuri ya Kiislamu mbali na kusema kuwa haibabaishwi na vitisho hivyo vya Marekani, imesisitiza kuwa kubakia Iran katika mapatano hayo ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kutategemea maamuzi ya nchi za Ulaya kuhusu kuipa Tehran dhamana madhubuti.

Tags

Maoni