Jun 07, 2018 03:17 UTC
  • Bunge la Iraq lataka zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi lirudiwe tena

Bunge la Iraq limeamua katika kikao cha dharura kilichofanyika hapo jana kuwa kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa bunge uliofanyika hivi karibuni zihesabiwe tena kwa mkono.

Kanali ya televisheni ya Al Alam imeripoti kuwa, katika kikao hicho kilichoongozwa na Spika Salim al Jabouri, Bunge la Iraq limesimamisha kazi iliyofanywa na Tume Kuu Huru ya Uchaguzi na kuamua kuunda jopo la majaji tisa wa kuchunguza mchakato mzima wa uchaguzi jinsi ulivyoendeshwa.

Duru ya kuaminika katika bunge la Iraq imezieleza duru za habari kuwa kikao hicho cha dharura cha bunge kilipiga kura ya kuidhinisha kuundwa tume hiyo ya kutafuta ukweli ili kuchunguza madai ya udanganyifu na ukiukaji taratibu uliofanywa katika mchakato mzima wa uchaguzi, kazi ambayo itahusisha vituo vyote vya upigaji kura nchini Iraq.

Mapema kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi alitangaza kuwa: serikali itachunguza kupitia kamati ya juu ya baraza la mawaziri malalamiko ya ukiukaji taratibu za uchaguzi ambayo yanadaiwa kufanywa katika uchaguzi wa bunge uliofanyika tarehe 12 ya mwezi uliopita wa Mei.

Zoezi la kuhesabu kura katika uchaguzi wa Iraq

Uchaguzi wa nne wa bunge la Iraq ulishirikisha miungano 27 na vyama 205 vya siasa vilivyowasilisha jumla ya orodha 88 za wagombea waliochuana kuwania viti 329 vya bunge la nchi hiyo.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume Kuu Huru ya Uchaguzi yameonyesha kuwa muungano wa Sairun unaoongozwa na Muqtada Sadr umepata viti vingi zaidi kwa kunyakua viti 54, ukifuatiwa na muungano wa Fat-h unaoongozwa na Katibu Mkuu wa harakati ya Badr Hadi Al-Amiri, ambao umepata viti 47.

Matokeo hayo aidha yameonyesha kuwa muungano wa An-Nasr unaoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo Haidar Al-Abadi umeshika nafasi ya tatu kwa kupata viti 43.../

Tags

Maoni