Jun 13, 2018 06:37 UTC
  • Jinamizi la kuendelea kupigwa Saudia kwa makombora ya Wayemen

Turki al Maliki, msemaji wa muungano vamizi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen ametangaza kuwa hadi sasa Wayemen wameshavurumisha makombora 149 upande wa Saudia.

Ripoti hiyo ya muungano wa Saudi Arabia kuhusu kuendelea kupigwa nchi hiyo kwa makombora ya wanamapambano wa Yemen na kukiri hadharani Riyadh kuwa wanamuqawama wa Yemen wana uwezo mkubwa wa makombora, ni uthibitisho tosha kuwa, nguvu za makombora ya Yemen mbali na kuvuruga mlingano wa kijeshi kwa madhara ya wavamizi wa nchi hiyo, pia zimezitia kihoro, woga na kitete nyoyo za wavamizi wa nchi hiyo ya Kiislamu. Bila ya shaka huo ni ushindi mwingine kwa mataifa yaliyosimama kidete kulinda haki zao katika eneo hili.

Turki al Maliki, msemaji wa muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen

 

Mwezi Machi 2015 Saudia iliunda muungano wa nchi kadhaa za Kiarabu kwa baraka kamili za Marekani na kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Yemen kwa tamaa ya kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu kwa hiari yake na kukimbilia Saudi Arabia. Tab'an ndoto hiyo ya Saudia haikutimia kama ambavyo siasa zake za kupenda kujitanua na kuvamia ardhi za nchi nyingine ambalo ndilo lengo kuu la kuvamiwa Yemen, nazo zimegonga mwamba. Licha ya wavamizi hao kufanya jinai na uharibifu wa kuchupa mpaka huko Yemen, lakini kila leo wanazidi kushindwa kwenye medani za mapambano na vipigo vya makombora vinaendelea kuindama Saudia bila ya kusita. Jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen wameamua kutumia stratijia ya mashambulizi ya makombora kwa ajili ya kuwalinda wananchi wasio na hatia wa nchi yao mbele ya uvamizi wa kijeshi wa ukoo wa Aal Saud na waitifaki wake hasa ukoo wa Aal Nahyan wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Kikosi cha makombora cha jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen wamepata mafanikio makubwa kwa kupiga wa ustadi wa hali ya juu maeneo muhimu ya Saudia. Wanamapambano hao wa Yemen wanafanya mashambulizi ya mtawalia katika miji ya mpakani ya Saudia na kuwasababishia hasara kubwa wanajeshi wa nchi hiyo vamizi na mamluki wao.

Hata hivi karibuni pia, jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vilitoa pigo kubwa kwa wavamizi wa nchi yao kiasi kwamba viongozi wa Imarati walimtumia jumbe kadhaa  mfalme wa Saudi Arabia na kumpa mkono wa pole kwa kuuliwa Wasaudia kadhaa katika mji wa mpakani wa Jizan. Jumbe hizo zenyewe zilitosha kuthibitisha uongo wa madai ya Wasaudia kuwa eti mfumo wa kujilinda kwa makombora wa Saudi Arabia una uwezo wa kutungua makombora ya Yemen. Hivi sasa ni vikosi vya muqawama vya Yemen ndivyo vilivyozitia kihoro na kitete roho za wavamizi wa nchi yao ambao wamekata tamaa na wanakiri mbele ya kadamnasi ya watu kuwa wameshindwa angalau kupunguza tu nguvu za makombora za jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen. 

Moja ya makombora ya Yemen likielekea Saudia. Uwezo wa kila namna wa makombora ya Yemen ni jinamizi kwa Saudi Arabia na wavamizi wenzake

 

Mwanzoni mwa vita hivyo vya kivamizi, Saudi Arabia ilijitokeza mbele ya hadhara ya walimwengu na kujigamba kuwa vita ilivyovianzisha Yemen havitachukua muda mrefu hata kidogo lakini leo hii inakiri mbele ya walimwengu kuwa imeshindwa kukabiliana na nguvu za makombora za Yemen tena basi ikiwa tumo ndani ya mwaka wa nne wa uvamizi huo. 

Salim Bashar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kimataifa wa Uturuki anasema: Vipigo vya mtawalia unavyopata utawala wa Aal Saud katika vita vyake na wananchi wa Yemen vimewatia kiwewe Wasaudia na kuwafanya wasijue cha kutenda. Jibu kali la muqawama wa wananchi wa Yemen linabainisha kuwa, pamoja na jinai zote zilizofanywa hadi hivi sasa na Saudia dhidi ya wananchi hao lakini imeshindwa kubadilisha mkondo wa kufeli na kushindwa kwake. Ni ukweli usiopingika kuwa, aina kwa aina ya nguvu za makombora ya muqawama wa wananchi wa Yemen zimekuwa ni jinamizi kwa utawala vamizi wa Saudi Arabia na marafiki zake wote.

Tags

Maoni