Jun 17, 2018 06:37 UTC
  • Kushadidi ukatili na jinai za Israel wakati wa kukaribia kutangazwa rasmi

Duru za habari zinaripoti kuwa mashambulio, jinai na ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina vimeshadidi katika wiki za karibuni sambamba na kukaribia kutangazwa rasmi na Marekani kile kilichopewa jina la "Mapatano ya Karne".

Katika miezi ya karibuni, utawala wa Kizayuni umeanzisha wimbi jipya la mashambulio ya anga dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza. Kushadidi jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni kunafanyika sambamba na harakati za Marekani za kutangaza rasmi na kuanza kuyatekeleza yale yanayotajwa kama "Mapatano ya Karne". Gazeti la Kizayuni la Israel Al-Yawm limezungumzia suala hilo kwa kuandika kuwa, Washington imemwita nyumbani balozi wake wa Israel kwa ajili ya kufanya mashauriano ya haraka kuhusu mpango eti wa amani uitwao "Mapatano ya Karne". Kwa mujibu wa gazeti hilo la Kizayuni, mpango uitwao "Mapatano ya Karne" takriban umeshakamilika kwa kufikia hatua yake ya mwisho ya maandalizi na huenda ukatangazwa hivi karibuni.

Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, mhusika mkuuu wa jinai na umwagaji damu za Wapalestina

Mpango huo umetayarishwa chini ya usimamizi wa tume maalumu ya Marekani inayoongozwa na Jason Greenblatt, mjumbe eti wa amani wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, balozi wa nchi hiyo katika utawala wa Kizayuni wa Israel David Friedman na Jared Kushner, mshauri mwandamizi wa rais Donald Trump wa Marekani. Kitambo nyuma balozi wa Marekani Israel David Friedman alitumia lugha ya vitisho kwa kusisitiza kwamba Mapatano ya Karne yameshakamilishwa na endapo Wapalestina hawatarejea kwenye meza ya mazungumzo na Marekani na utawala wa Kizayuni, hatua yao hiyo itawagharimu pakubwa. Ni kufuatia vitisho hivyo ndipo lilipoanza wimbi jipya la jinai na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina. 

Kutoka kushoto: Greenblatt, Friedman na Kushner wakiwa pamoja na Netanyahu

Mpango eti wa amani wa Trump unaotajwa kuwa ni wa Mapatano ya Karne ni mpango unaowiyana kikamilifu na malengo na matakwa ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Kizayuni, pasi na kujali wala kuzingatia kwa namna yoyote ile matakwa na haki za Wapalestina. Ikiwa mpango wa Mapatano ya Karne utatekelezwa, kabla ya jambo lolote lile, Wapalestina wataipoteza moja kwa moja Quds tukufu, haki ya wakimbizi wa Kipalestina ya kurejea kwenye miji na maskani yao ya asili itabaki kuwa ndoto ya milele na Wapalestina watazidi kuandamwa na sera za kibaguzi za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Watoto wa Kipalestina wakisisitiza kuwa Quds ni mji mkuu wa Palestina

Katibu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukomboki wa Palestina PLO amesema kuhusiana na suala hilo kuwa viongozi wa Palestina wameshatangaza kuwa wanaupinga mpango uitwao Mapatano ya Karne na wala hawasubiri kutolewa ufafanuzi wake. Saeb Erekat amesisitiza kuwa kitendo cha Marekani cha kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wake wa Tel Aviv kinalenga kufuta haki za Wapalestina. Erekat ameongeza kuwa: Lengo la mpango uitwao Mapatano ya Karne ni kuhalalisha siasa za ubaguzi wa rangi za Wazayuni na ujenzi wa vitongoji wa utawala huo kwa kufuata vigezo na viwango vya Marekani. 

Saeb Erekat

Tunapoyahakiki matukio yanayojiri Palestina tangu baada ya Trump kuingia madarakani tutabaini kuwa hatua za ukatili, jinai na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zimechukua wigo mpana na wa kutisha zaidi kutokana na mwenendo na mipango ya kiadui ya Trumo na kutangazwa uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani kwa Israel. Ni katika mazingira kama hayo na kwa baraka kamili za Marekani, na kwa kutumia tajiriba ya Washington ambayo ina rekodi ndefu na uzoefu mkubwa wa kuyakandamiza mataifa mengine na kuamiliana kiubaguzi na raia wake wake yenyewe, ndipo tunashuhudia utawala wa Kizayuni ukiandaa na kuratibu ramani ya njia inayolenga kuwakandamiza zaidi Wapalestina na kulizima vuguvugu la Intifadha.

Matokeo ya siasa za aina hii na upangaji njama wa pamoja wa Washington na Tel Aviv ni kushadidi mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na Israel sambamba na kampeni inayoendeshwa na Marekani ya kuzusha hofu na kutoa vitisho kwa madhumuni ya kuzikubalisha nchi za eneo mpango wake wa Mapatano ya Karne. Ni kupitia mpango huu, Marekani imedhamiria kuifuta Palestina kwenye ramani ya kisiasa ya dunia; na kwa kampeni ya vitisho inayoendesha imeandaa mazingira ya kushadidishwa jinai na ukatili wa utawala dhalimu wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.../ 

Maoni