Jun 17, 2018 07:22 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyateka meli ya kivita ya wavamizi katika Bandari ya Al Hudaydah

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen ametangaza mapema Jumapili kuwa vikosi vya Yemen vimeteka meli moja ya kivita ya majeshi vamizi katika pwani ya bandari ya al Hudaydah.

Mohammed Ali al-Houthi  amesisitiza kuwa wavamizi wanakabiliwa na hali ngumu katika mwambao wa kusini mwa Hudaydah na kuongeza kuwa: 'Yamkini meli hiyo ya kivita ni ya Ufaransa au Marekani."

Mohammed Ali al-Houthi ameongeza kuwa, mwambao wa al Hudaydah utageuka na kuwa kaburi la wavamizi.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia Arabia, kuanzia Jumatano Juni 13, ulianzisha mashambulizi makubwa kwa lengo la kuteka na kukalia kwa mabavu mji wa bandaraini wa al Hudaydah wa magharibi mwa Yemen.

Bandari ya al Hudaydah ni njia kuu inayotumika kuingiza misaada ya kibinadamu nchini Yemen. Umoja wa Mataifa umebainisha wasiwasi wake kuhusu yanayojiri katika bandari ya al Hudaydah. Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Yemen imesema Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani zinabeba dhima ya kushambulia na kuharibu miundo msingi ya kiafya katika Bandari ya al Hudaydah.

 

Mohammed al Houthi Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen

Saudia kwa kushirikiana na Marekani na Israel ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani na kibaraka wa Riyadh aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutoroka nchi. Hadi sasa mashambulizi hayo yameua zaidi ya watu elfu 14 na kuujeruhi makumi ya maelfu ya wengine wengi wao wakiwa ni watoto wadogo na wanawake.

Kadhalika hujuma hizo za kinyama zimesababisha mamilioni ya raia wa taifa hilo kuwa wakimbizi. Hata hivyo licha ya nchi vamizi kutumia kila aina ya silaha dhidi ya Yemen, zimeshindwa kufikia malengo yao na hivyo kuzifanya zinase katika kinamasi nchini humo.

Maoni