Jun 18, 2018 07:31 UTC
  • Hamas yavurumisha maroketi kujibu jinai za Israel, ving'ora vyahinikiza vitongoji vya Wazayuni

Wanamapambano wa Palestina wamevurumisha maroketi matatu kupiga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni baada ya ndege za kivita za Israel kufanya mashambulizi katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ghaza mapema leo asubuhi na kuongeza wasiwasi wa kutokea vita vipya katika ukanda huo uliozingirwa kila upande.

Shambulizi hilo limepelekea kusikika mara kadhaa ving'ora vya tahadhari katika eneo la Hof Ashkelon, eneo la viwandani la Ashkelon, Kibbutz Yad Mordechai na Netiv Ha'asara na kuwalazimisha maelfu ya walowezi wa Kizayuni kukimbilia kwenye mahandaki.

Magazeti ya Israel yamesema kuwa, maroketi mawili yametua ndani ya Israel wakati la tatu limetunguliwa kabla ya kupiga shabaha. Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu hasara zilizosababishwa na mashambulizi ya pande hizo mbili.

Mpalestina akirusha maputo kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Wazayuni wanavyopenda dunia, hata maputo meupe yasiyo na kitu wanaona ni jinamizi kwao

 

Wanamapambano wa Palestina wamelazimika kurusha maroketi hayo kujibu mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za Israel kaskazini mwa ukanda wa Ghaza mpema leo asubuhi katika juhudi za Wazayuni za kuwazuia Wapalestina wasirushe maputo na vishada vyenye moto kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. 

Vyombo vya habari vya Israel vimesema kuwa, huenda utawala wa Kizayuni ukaanzisha mauaji kutokea angani ikiwa ni pamoja na kumshambulia yeyote atakayeonekana na kishada au puto. 

Jana, afisa mmoja wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni alisema kuwa, kama utawala huo utazidi kuwashambulia Wapalestina basi mashambulizi hayo yanaweza kuzusha vita vipya katika Ukanda wa Ghaza baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Vishada na maputo yenye moto yamekuwa ni silaha mpya za Wapalestina za kukabiliana na mauaji na jinai wanazofanyiwa na Wazayuni ambao wamezidi kuwaua kiholela Wapalestina wanaofanya maandamano ya amani tangu tarehe 30 Machi mwaka huu.

Maandamano ya Wapalestina hao yalishika kasi tarehe 14 Mei wakati wakazi 40 elfu waliposhiriki katika maandamano hayo katika mpaka wa kaskazini mwa Ghaza kulalamikia jeuri ya Marekani ya kufungua ubalozi wake huko al Quds baada ya kuutambua rasmi mji huo mtakatifu wa Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel.

Maoni