Jun 18, 2018 15:21 UTC
  • Makumi ya vibaraka wa Saudia na makamanda wao waangamizwa al Hudaydah, Yemen

Makumi ya vibaraka wa Saudi Arabia wakiwemo makamanda wao kadhaa katika uwanja wa vita, wameangamizwa katika mapigano makali yanayoendelea eneo la pwani ya magharibi mwa Yemen, al Hudaydah sambamba na mamia kati yao kujeruhiwa.

Kanali ya televisheni ya al-Alam imeripoti kwamba jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah, limefanikiwa kuteketeza magari 44 ya kijeshi na ya deraya ya vibaraka hao. Kadhalika katika operesheni za kushambulia eneo la jimbo la Dhale, kusini mwa Yemen, jeshi hilo na wanamapambano wa Answarullah wamefanikiwa kuangamiza na kujeruhi idadi nyingine ya vibaraka hao wa utawala wa Aal-Saud katika maeneo ya Jamash, Hajalan na Maris.

Askari vamizi wa Imarati wakiwa na kamanda wao ambao wameangamizwa

Ali Qashr, Naimu Gavana wa mkoa wa al Hudaydah na Mkuu wa Baraza la Mshikamano wa Makabila ya Yemen pia amethibitisha kuangamizwa Isa Seif Bin Abalan al-Mazrui, naibu kamanda mkuu wa vikosi vya jeshi la Imarati na kundi la maafisa wa nchi hiyo waliouawa katika mapigano ya siku mbili zilizopita eneo la magharibi mwa Yemen. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Yemen, idadi ya askari na vibaraka wa muungano wa Saudia waliouawa katika kipindi cha siku chache zilizopita imefikia 253 huku serikali ya Imarati nayo ikikiri kuuawa askari wake kadhaa huko al Hudaydah na maeneo mengine ya Yemen. Kufuatia kudhibitiwa na wanamuqawama wa Yemen meli moja ya kivita katika maji ya al Hudaydah, duru moja ya habari mapema leo nchini Yemen imetangaza kuwa, askari waliokuwa ndani ya meli hiyo wana uraia wa Ufaransa na kwamba walikuwa wakifanya ujasusi katika pwani ya nchi hiyo kwa maslahi ya muungano vamizi wa Saudia, Marekani, Israel na Imarati.

Jeshi la Yemen ambalo limeapa kusimama imara dhidi ya wavamizi

Aidha duru moja mjini al Hudaydah sambamba na kutangaza kwamba hivi sasa kunapiganwa vita vya dunia dhidi ya watu wa Yemen, amesema, mbali na wavamizi wa Saudia na Imarati na vibaraka wao, mashirika ya mataifa kadhaa, askari wa Marekani, Israel, Ufaransa na Uingereza wanashirikiana bega kwa bega na Saudia katika vita hivyo dhidi ya taifa hilo masikini la Yemen.

Maoni