Jun 20, 2018 13:36 UTC
  • Udharura wa dunia kuzingatia kadhia ya wakimbizi wa Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, imesisitiza kuwa, jukumu la kutetea haki zote za kisiasa na kifedha za wakimbizi Wapalestina ni la jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne sambamba na kuanza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Shirika la Umoja wa Mataifa Linalowasaidia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA,  huko Amman, mji mkuu wa Jordan, Hamas imesema: "Kuibua changamoto katika faili la wakimbizi Wapalestina, ni jambo ambalo si tu kwamba litakuwa na taathira hasi katika ardhi za Palestina  bali pia litasababisha ukosefu wa usalama katika eneo."

Idadi ya wakimbizi Wapalestina hivi sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni sita. Idadi  hiyo inabeba asilimia kubwa ya wakimbizi duniani na ni ishara ya ukubwa wa maafa ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel umewasababishia Wapalestina.

Katika hali ambayo Wapalestina wanakabiliwa na njama ya kuwanyima haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi, wanakabiliwa pia na dhulma nyinginezo nyingi. 

Wasiwasi wa Wapalestina na walimwengu umeongezeka kuhusu kadhia ya wakimbizi Wapalestina baada ya kubainika kuwa kupuuza au kujaribu kuzima kadhia hiyo ni kati ya njama kuu za Rais Donald Trump wa Marekani ambaye analenga kuwakandamizwa Wapalestina kupitia kile anachodai kuwa eti ni 'Mapatano ya Karne."

Hivi sasa Marekani imeshaanza kutekeleza kivitendo njama yake hiyo mpya.

Katika fremu hiyo, sambamba na kufanyika kongamano linalohusu wakimbizi Wapaletina nchini Jordan, Jared Kushner mshauri wa ngazi za juu na mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na Jason Greenblatt mjumbe maalumu wa Trump katika mazungumzo eti ya maelewano  Mashariki ya Kati, walikutana na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan mjini Amman. Duru za habari Marekani zimetangaza kuwa, maudhui kuu katika mkutano huo ilikuwa ni mchakato wa nchi za eneo kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika fremu ya 'Mapatano ya Karne."

Makao makuu ya UNRWA katika Ukanda wa Ghaza

Matukio ya eneo yanaonesha kuwa Marekani inatekeleza njama mpya nyuma ya pazia dhidi ya Wapalestina hasa kuhusu kadhia ya wakimbizi Wapalestina.

Ni kwa msingi huo ndio Israel ikaanzisha duru mpya ya kukandamiza haki za Wapalestina katika kufuata propaganda za Marekani za kujaribu kuvuruga malengo matukufu ya taifa la Palestina, hasa kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu.

Katika hali kama hii Wamarekani pia wamekuwa wakifuatilia maudhui ya kile wanachotaja kuwa ni nchi na ardhi mbadala ya Wapalestina. Ni katika fremu hiyo ndio tunaweza kutathmini hatua ya utawala wa Trump kupinga vikali haki ya Wapalestina kurejea katika ardhi zao za jadi pamoja na sera zake za kichochezi kuhusu Quds.

Tukiangazia mpango wa Marekani dhidi ya Wapalestina wa 'Mapatano ya Karne'  tunaweza kufikia natija kuwa, mpango huo una lengo la kukamilisha njama za huko nyuma za Marekani na  baadhi ya madola ya Kiarabu kuhusu kadhia ya Palestina ambazo zilikuwa zikitekelezwa katika fremu ya kuanzisha uhusiano na malewano na utawala wa Kizayuni.

Wapalestina katika maandamano ya kutetea haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi huko Ghaza

Chokochoko mpya za Marekani na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kukandamiza haki ya kurejea Wakimbizi Wapalestina inatekelezwa katika hali ambayo maazimio ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na azimio nambari 194 la Umoja wa Mataifa yamebainisha wazi haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea katika ardhi zao zote za jadi sambamba na kulipwa fidia ya hasara walizopata kwa kuporwa ardhi zao.

Kutokana na jamii ya kimataifa kutozingatia kwa kina haki za Wapalestina, zikiwemo haki za wakimbizi na mateka Wapalestina, walimwengu wanaendelea kushuhudia Wapalestina wakisalia kuwa wakimbizi na masaibu yao yanaongezeka siku baada ya siku. Inatarajiwa kuwa, jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa utaachana na misimamo yake legevu na kuchukua hatua za kimsingi na kivitendo kwa lengo la kutekeleza maazimio ya kimataifa ili kuwapa haki zao wakimbizi Wapalestina.

Tags

Maoni