• Kushindwa muungano wa kijeshi wa Saudia katika bandari ya al-Hudaidah

Muhammad Abdu as-Salaam, msemaji rasmi wa harakati ya Ansarullah ya nchini Yemen ametangaza habari ya kushindwa operesheni za kijeshi zilizoanzishwa na muungano wa kichokozi unaoongozwa na Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala haramu wa Isrseal, Ufaransa na Uingereza katika bandari ya nchi hiyo ya al-Hudaidah.

Picha zinazoonyesha viongozi wa Yemen na wa harakati ya Ansarullah wakitembea na kuukagua uwanja wa ndege wa al-Hudaidah kwa hakika zinadhihirisha wazi kushindwa muungano huo wa kijeshi wa Saudia kufikia malengo yake ya kutaka kuliteka eneo hilo la kistratijia ukiwemo uwanja wake wa ndege, kama ulivyokuwa ukidai hapo awali kuwa ulikuwa umeuteka uwanja huo wa ndege. Ripoti kutoka medani ya vita ya Yemen zinathibitisha wazi kwamba muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umeshindwa tena katika wimbi jipya la mashambulio yake ya kijeshi huko al-Hudaidah na hivyo kuendelea kukwama katika kinamasi cha Yemen. Licha ya kutolewa tahadhari na taasisi za kimataifa kuhusiana na janga na maafa ya kibinadamu yanayoweza kusababishwa na wimbi hilo jipya la mashambulio ya kichokozi ya Saudia katika bandari ya al-Hudaidah, lakini nchi hiyo  ikishiriana na vibaraka wake ilianzisha hujuma kali ya kijeshi katika bandari hiyo wiki kadhaa zilizopita, kwa ajili ya kufunika aibu ya kushindwa kwake kijeshi katika maeneo mengine ya Yemen na sasa imebainika wazi kwamba imepata pigo jingine la kufedheheshwa kijeshi na jeshi pamoja na harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Saudia yapata maafa na hasara kubwa  Yemen

Muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen umepata hasara na maafa makubwa katika safu za askari jeshi wake kutokana na mapigo ya jeshi na harakati ya Ansarullah, katika hali ambayo unapata uungaji mkono mkubwa wa kijeshi kutoka nchi za Magharibi. Mapambano ya watu wa Yemen yamethibitisha wazi kwamba hujuma na uchokozi wa Muungano wa Saudia dhidi ya Wayemen hautakuwa na natija nyingine ghairi ya kuendelea kufedheheshwa kijeshi nchini humo. Yakiakisi mapigo ya kijeshi ambayo Saudia imekuwa ikiyapata katika ardhi ya Yemen na hasa pigo la hivi karibuni katika bandari ya al-Hudaidah, magazeti ya al-Binaa na Rai' al-Yaum ya nchini Lebanon, Swaut al-Iraq la Iraq na al-Manar la Palestina yametabiri kwamba Saudia itashindwa vibaya hivi karibuni na hivyo huo kuwa mwanzo wa kusambaratika utawala wa Aal Saud huko Saudi Arabia. Nchi hiyo ambayo imekuwa ikiendesha mashambulio ya kijeshi nchini Yemen tokea tarehe 26 Machi 2015 ilidhani kwamba ingeweza kuwashinda wapiganaji wa Ansarullah kwa haraka na hivyo kuiwezesha kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdu Rababuh Mansur Hadi, rais wa zamai wa Yemen aliyejiuzulu na kuikimbia nchi kutafuta hifadhi huko Saudia, lakini kinyume na dhana hiyo, vita hivyo sasa vimeingia katika mwaka wake wa nne hali ya kuwa haijafikia hata lengo moja kati ya malengo yaliyoipelekea kuanzisha vita hivyo vya kichokozi dhidi ya jirani yake huyo masikini.

Uharibifu mkubwa unaosababishwa na hujuma ya kichokozi ya Saudia nchini Yemen

Kuharibu zaidi hali ya mambo ni kuwa, Saudia imetumbukia katika kinamasi kipya katika bandari ya al-Hudaidah baada ya kufedheheshwa vibaya kijeshi katika hujuma iliyoianzisha katika bandari hiyo zaidi ya mwezi mmoja uliopita. Kutokana na uungaji mkono mkubwa wa kijeshi inaopata kutoka kwa utawala haramu wa Israel, Marekani, Ufaransa na Uingereza, Saudia ilikuwa imepanga kuteka uwanja wa ndege na bandari ya al-Hudaidah kabla ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani lakini sasa hilo limegeuka na kuwa ndoto tu isiyothibiti. Ndoto hiyo inakumbusha ndoto nyingine ya Saudia ambayo mwanzoni mwa hujuma yake ya kichokozi dhidi ya Yemen  mwezi Machi 2015 ilikuwa imepanga kuteka  na kuidhibiti ardhi yote ya Yemen katika kipindi cha mwezi mmoja. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa hujuma ya kijeshi ambayo ilikuwa imepangwa na Saudia, Imarati na washirika wao wa kigeni kuwaletea ushindi wa dhahabu nchini Yemen sasa imebadilika na kuwa mfano halisi wa kushindwa kukubwa na kuchungu kijeshi katika nchi hiyo.

Jun 22, 2018 13:18 UTC
Maoni