• Jeshi la Syria lazingira ngome ya jeshi vamizi la Marekani katika mpaka wa Iraq

Sambamba na operesheni ya kuyasafisha maeneo mapana ya jangwa la Syria, hasa eneo la al-Badiya kutoka mikononi mwa mabaki ya wanachama wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), jeshi la Syria limezingira ngome ya askari vamizi wa Marekani katika eneo la al-Tanf lililopo katika mpaka wa nchi hiyo na Iraq.

Taarifa iliyotolewa leo imesema kuwa, kuzingirwa kwa kambi hiyo ya jeshi la Marekani kumejiri baada ya operesheni pana ya jeshi la Syria ya kuyasafisha maeneo ya viunga vya mji wa Damascus, Homs na Deir ez-Zor na pia kukombolewa maeneo zaidi ya kilomita mraba 4000 katika jangwa la nchi hiyo. Askari vamizi wa Marekani walitia kambi katika eneo la al-Tanf lililoloko katika mpaka wa Iraq na Syria bila ya idhini ya serikali ya Damascus kwa lengo la kuendelea kutoa msaada wa silaha na kilojestiki kwa mabaki ya wanachama wa kundi la Daesh (ISIS). Kadhalika baada ya jeshi la Syria kushambulia magari matatu ya askari wa Marekani kusini mashariki mwa mji wa Palmyra katika mkoa wa Homs, kulianza mapigano ya nchi kavu kati ya jeshi la Syria na askari wa muungano vamizi wa kimataifa unaodaiwa eti kuwa dhidi ya Daesh unaoongozwa na Marekani nchini Syria.

Askari wa Marekani waliozingirwa na jeshi la serikali halali ya Syria

Itakumbukwa kuwa Marekani na washirika wake waliunda muungano wa kimaonyesho kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) mwaka 2014, muungano ambao tangu kuundwa kwake umejikita tu katika kuishambulia miji ya Syria na kuwalenga askari wa serikali na raia wa nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa mara kadhaa serikali ya Syria imekuwa ikipinga uwepo wa jeshi la Marekani ndani ya ardhi ya nchi hiyo na kuuitaja kuwa ni uvamizi dhidi ya nchi huru. Wakati huo huo jeshi la Syria limefanikiwa kuangamiza idadi kadhaa ya mabaki ya wanachama wa Daesh katikati ya jangwa la Sakhnah viungani mashariki mwa mkoa wa Homs nchini humo.

Tags

Jun 22, 2018 14:07 UTC
Maoni