• Taleban: Helikopta za Marekani zinawasaidia wanachama wa Daesh dhidi yetu

Kundi la kigaidi la Taleban nchini Afghanistan limesema kwamba helikopta za kijeshi za Marekani zimekuwa zikiwasaidia wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika uwanja wa vita kati ya wanachama wa makundi hayo sambamba na kushambulia ngome za Taleban katika mkoa wa Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo.

Zabiullah Mujahid, Msemaji wa Kundi la Taleban ameongeza kwamba, katika vita vinavyoendelea kati ya kundi hilo na lile la Daesh (ISIS), helikopta za kijeshi za Marekani zimekuwa zikiingilia kati kwa ajili ya kutoa msaada kwa wanachama wa Daesh. Amesema, ndege hizo pia zimekuwa zikifanya mashambulizi kuzilenga ngome za Taleban na kuua wanachama wengi wa kundi hilo. Zabiullah Mujahid ameongeza kwamba, siku chache zilizopita wanachama wa genge la Daesh waliwasili katika kijiji cha Alingar ndani ya mkoa wa Nangarhar na kuanzisha ngome zao eneo hilo. Hii sio mara ya kwanza kwa kundi la Taleban na baadhi ya viongozi wa Afghanistan kutangaza kwamba Marekani imekuwa ikiwasaidia wanachama wa genge la Daesh nchini humo.

Kundi la kigaidi la Daesh

Mwezi Mei mwaka jana serikali ya mkoa wa Nangarhar ilitangaza kuwa, askari wa Marekani waliwaokoa wapiganaji wa ISIS waliokuwa wamezidiwa nguvu na kuzingirwa na wanamgambo wa Taleban katika mji wa Chaparhar wa mkoa tajwa. Taarifa iliyotolewa na serikali ya mkoa huo ilisema kuwa, ni suala lisilo na shaka kwamba hatua hiyo ya Washington kwa magaidi hao wa Daesh iliratibiwa moja kwa moja na White House kwa ajili ya kulitumia genge hilo kufikia malengo yake nchini Afghanistan na katika eneo.

Tags

Jun 23, 2018 02:23 UTC
Maoni