Jul 11, 2018 04:08 UTC
  • Takwa la kukomeshwa mauaji dhidi ya watoto nchini Yemen

Waziri Mkuu wa Sweden ametoa wito wa kuhitimishwa jinai za utawala wa Saudi Arabia huko nchini Yemen.

Stefan Löfven amesema hayo baada ya kumalizika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likichobeba anwani isemayo "Kuwalinda Watoto Katika Machafuko". Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamepasisha kwa kauli moja katika kikao hicho azimio la kuwalinda watoto katika vita na mapigano ya utumiaji silaha.

Kwa mujibu wa azimio hilo, watoto wanapaswa kusalimika na aina yoyote ile ya utumiaji mabavu. Aidha azimio hilo linapiga marufuku kutumiwa watoto kama askari vitani, kuwaua, kuwateka nyara, kuwatumia kingono, kushambuliwa shule na hospitali. Azimio hilo kadhalika linasema kuwa, kuzuia shughuli za ufikishaji misaada ya kibinadamu ni kukiuka wazi sheria za kimataifa.

Stefan Löfven, Waziri Mkuu wa Sweden

Suala la kuwalinda watoto katika machafuko na vita linazungumziwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika hali ambayo, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ni kuwa, mwaka uliopita wa 2017 pekee zaidi ya watoto elfu kumi waliuawa au kukatika viungo katika maeneo tofauti ulimwenguni kwa sababu ya vita na mapigano ya kutumia silaha. Watoto wa Yemen ni miongoni mwa wahanga wakuu wa jinai za kivita ambapo Saudi Arabia, Imarati na washirika wao wameanzisha vita dhidi ya wananchi wa taifa hilo masikini la Kiarabu.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto milioni 11 wa Yemen wanahitaji misaada ya kibinadamu kutokana na athari mbaya ambazo zimesababishwa na hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake. Saudia na waitifaki wake wanaendelea na hujuma zao za kijeshi nchini Yemen katika hali ambayo, hadi sasa wameshindwa kabisa kufikia malengo yao waliojipangia.

Hivi sasa madola waitifaki katika vita hivyo yameshadidisha mauaji dhidi ya watoto wa Yemen na kuzuia kufikishiwa misaada ya kibinadamu wananchi wa nchi hiyo kama chakula na dawa ili kwa njia hiyo asaa rais hao watasalimu amri mbele ya siasa za kupenda kujitanua za Riyadh.

Masaibu ya watoto wa Yemen

Nukta ya kutilia maanani katika suala hili ni uungaji mkono wa madola ya Magharibi na utawala haramu wa Israel kwa Saudia na washirika wake katika vita dhidi ya Yemen pamoja na undumakuwili wa madola hayo. Katika hali ambayo, akthari ya madola hayo yamekuwa yakitoa matamshi ya kupinga mauaji dhidi ya watoto wa Yemen yanayofanywa na Saudia na waitifaki wake na hata wakati mwingine kuyalaani, lakini ni madola hayo hayo ambayo yamekuwa yakiiunga mkono Saudia kisiasa na ndio wauzaji wakubwa wa silaha kwa utawala wa Riyadh na marafiki zake.

Bénédicte Jeannerod, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamuu la Huuman Rights Watch nchini Ufaransa anasema: Saudia inaongoza muungano wa kijeshi ambao hadi sasa umeua maelfu ya raia nchini Yemen, mauaji ambayo akthari yake yanapaswa kuhesabiwa kuwa ni jinai za kivita. Ikiwa Ulaya itaendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia itakuwa mshirika wa jinai za kivita na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen

Kwa hakika hatua ya Marekani na madola ya Ulaya ya kuiuzia silaha na zana za kivita Saudi Arabia, kuziunga mkono siasa za kivamizi za Riyadh katika Mashariki ya Kati  na vita vyake nchini Yemen imepelekea maelfu ya raia wa Yemen hususan watoto wakabiliwe na mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaotokana na uhaba wa dawa, chakula na kuishi katika mazingira yasiyo salama.

Hatua ya viongozi wa Riyadh ya kung'ang'ania kusukuma mbele gurudumu la siasa zao huko Yemen imezidi kuyafanya mazingira inayokabiliwa nayo nchi hiyo kuharibika zaidi. Katika mazingira kama haya, watoto wangali wahanga wakuu ambapo kutolewa tu maazimio na asasi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katu hakuwezi kubadilisha na kuboresha hali yao, bali kukatwa misaada na kusimamishwa uungaji mkono wa nyuma ya pazia wa Magharibi kwa Saudi Arabia na washirika wake na wakati huo huo kushinikizwa Riyadh ili ihitimishe vita vyake huko Yemen, ni hatua ambazo angalau zinaweza kwa kiwango fulani kurejesha usalama wa watoto wa nchi hiyo.

Maoni