Jul 11, 2018 07:34 UTC
  • Utawala wa Aal-Khalifa, unapaswa kuwajibika kuhusu usalama wa Sheikh Isa Qassim, kiongozi mkubwa wa Bahrain

Katika siku za hivi karibuni waandamanaji wa Bahrain sambamba na kupiga nara za kuulaani utawala wa kifalme wa Bahrain, wameutaja utawala huo kuwa mbeba dhima wa hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Isa Qassim na kutaja madai ya mfalme wa nchi hiyo kuwa anafanya juhudu za kumtibu mwanazuoni huyo, kuwa ni uongo mtupu.

Katika siku kadhaa zilizopita, Wabahrain wameuonya utawala wa nchi hiyo juu ya kutumia vibaya hali mbaya ya kiafya ya kiongozi huyo wa kidini. Baada ya hali ya Sheikh Isa Qassim kuwa mbaya na kadhalika kushtadi malalaimiko ya wananchi katika kulaani kifungo cha nyumbani dhidi ya mwanazuoni huyo hatimaye Hamad bin Isa Al Khalifa, Mfalme wa Bahrain ametoa amri na chini ya uangalizi wa madaktari, kupelekwa nje ya nchi mwanazuoni huyo kwa ajili ya kupata matibabu. Raia wa Bahrain wana wasi wasi kwamba baada ya utawala wa nchi hiyo kuruhusu shakhsia huyo kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, baadaye utamzuia kurejea nchini na hivyo kutekeleza hukumu ya kidhalimu na iliyo kinyume cha sheria ya kumvua uraia wake.

Sheikh Isa Qassim, akiwa katika hali mbaya kiafya

Ili kujibu swali la ni namna gani Sheikh Isa Qassim ameweza kuruhusiwa kutoka nje ya nchi na kwa kuzingatia kwamba tayari amekwishavuliwa uraia na utawala wa nchi hiyo, Mfalme wa Bahrain amesema kuwa serikali imemtengenezea pasi ya muda mfupi ya kusafiria kwa ajili ya shughuli hiyo, na kwamba hata hivyo kitambulisho hicho hakionyeshi kuwa bado ni raia wa Bahrain, bali kinaonyesha tu eneo analoishi nchini humo. Wanaharakati wa kisiasa nchini humo wametahadharisha juu ya uwezekano wa utawala wa nchi hiyo kumbaidisha mwanazuoni huyo nje ya nchi. Hata hivyo kile ambacho kinawatia wasi wasi mkubwa wafuasi wake kwa sasa ni usalama wa afya yake na masuala mengine yanachukua nafasi ya pili. Alaa kulli hal, utawala wa Bahrain ndio mbeba dhima wa afya ya Sheikh Isa Qassim na hivyo unapaswa kuwajibishwa kuhusiana na jambo lolote litakalompata mwanazuoni huyo. Ukweli ni kwamba kuzorota kwa hali ya kiafya ya mwanazuoni huyo kumetokana na sababu mbalimbali zikiwemo za utawala huo wa kiimla kumzuia mwanazuoni huyo kupata matibabu kwa wakati unaofaa na vilevile kuwazuia watu wa karibu yake kufuatilia hali yake ya kiafya sambamba na kuendelea kuzingirwa makazi yake na maafisa usalama wa nchi hiyo.

Sheikh Isa Qassim, kipenzi cha Wabahrain

Hii ni katika hali ambayo weledi wa mambo wanaamini kwamba mashinikizo ya kiroho na kimwili yaliyofanywa na utawala wa Aal-Khalifa, dhidi ya mwanazuoni huyo, ndicho chanzo cha kuzorota hali yake ya kiafya na kushtadi maradhi yake. Baadhi ya weledi wa masuala ya kiasiasa hawapingi uwezekano kwamba huenda utawala huo umehusika na njama maalumu ya kumuambukiza maradhi hatari Sheikh Isa Qassim, hasa kwa lengo la kumuondoa katika uwanja wa matukio ya Bahrain. Raia wa Bahrain walianzisha maandamano ya amani Februari 2011 wakidai uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kubuniwa serikali iliyochaguliwa na wananchi. Hata hivyo utawala huo badala ya kutekeleza matakwa hayo ya wananchi, uliamua kuwatia mbaroni viongozi wa upinzani sambamba na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu. Muamala mbaya wa utawala huo dhidi ya Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni na kiongozi mkubwa wa mwamko wa wananchi, unabainisha wazi kiwango kikubwa cha ukandamizaji unaotekelezwa na utawala huo wa Aal-Khalifa dhidi ya raia wake. Kuhusu suala hilo, Jalal Firuz, mbunge wa zamaniwa Bahrain na mmoja wa wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo, anatahadharisha kwamba iwapo Sheikh Isa Qassim ataaga dunia, jambo hilo linaweza kuwa na matokeo mabaya ya siasa kwa serikali ya Manama. Kile kilicho wazi ni kwamba jambo lolote baya litakalomsibu mwanazuoni huyo, linaweza kuripua moto wa hasira za wananchi na hivyo kuvuruga hali ya mambo nchini humo.

Maoni