Jul 11, 2018 12:41 UTC
  • Shambulio la nne la ufyatuaji risasi mjini Riyadh katika muda wa miezi 7; kuongezeka hali ya mchafukoge

Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa mtu mmoja asiyefahamika aliyekuwa na silaha ya moto jana usiku aliingia kwenye hospitali ya Mfalme Salman huko Riyadh mji imkuu wa Saudi Arabia na kuanza kuwamiminia risasi wafanyakazi wa kitengo cha uuguzi. Katika tukio hilo muuguzi mmoja alijeruhiwa pakubwa huku mvamizi aliyekuwa na risasi pia akifanikiwa kukimbia.

Baada ya kuteuliwa Muhammad bin Salman kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia; nchi hiyo sasa inakabiliwa na matatizo mbalimbali ya ukosefu wa usalama wa ndani.

Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia 

Kuna ushahidi mkubwa na wa wazi  kuhusiana na suala hilo ambapo vitendo vya ufyatuaji risasi katika maeneo mbalimbali ya umma ni moja ya matukio hayo. Polisi nchini Saudia mwezi Disemba mwaka jana iliripoti kujiri ufyatuaji risasi karibu na msikiti mmoja katikati mwa mji mkuu Riyadh ambapo raia mmoja wa Saudia aliuliwa. 

Shambulio la ufyatuaji risasi msikitini mjini Riyadh Saudi Arabia 

Mwezi Aprili mwaka huu pia kulijiri ufyatuaji mwingine wa risasi kandokando ya ikulu ya Mfalme Salman huko Riyadh; ambapo ripoti ziliarifu kuwa watu 8 waliuawa na hata kupelekea kuenea tetesi kwamba Muhammad bin Salman pia alikuwa amejeruhiwa katika tukio hilo. Aidha siku tatu zilizopita yaani tarehe 8 mwezi huu wa Julai Mansour al Turki Msemaji wa Masuala ya Usalama wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia alitangaza kuwa kituo kimoja cha usalama katika barabara ya Buraidah al Tarifiya katika eneo la al Qassim kaskazini mwa Riyadh kilishambuliwa kwa risasi. Wavamizi wawili na polisi mmoja walipoteza maisha katika tukio hilo la ufyatuaji risasi. Ufyatuaji risasi uliotekelezwa jana usiku katika hospitali ya Mfalme Salman pia ni wa nne kujiri katika mji mkuu Riyadh katika muda wa miezi saba iliyopita na katika maeneo ya karibu yake. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya maeneo mengine ya Saudi Arabia yakiwemo maeneo ya mashariki mwa nchi pia katika miezi ya karibuni yamekumbwa na matukio ya ufyatuaji risasi. 

Matukio hayo yote yanadhihirisha kuongezeka ukosefu wa usalama nchini Saudia khususan katika mwaka mmoja wa uliopita. Muhammad bin Salman mwezi Juni mwaka jana aliteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Matukio hayo yamebadilisha ugawanaji wa madarakani nchini Saudia. Hii ni kwa sababu wasia ulioachwa na Abdulazizi mwasisi wa utawala wa Aal Saud unaeleza kuwa madaraka nchini humo yanatakiwa yakikabidhiwe kwa usawa kutoka kaka mmoja kwenda kwa mwingine, hata hivyo katika kipindi hiki cha uwepo wa mrithi wa kiti cha ufalme Muhammad bin Salman na shakhsia huyo kuwa na nafasi kubwa ya kukalia kiti cha ufalme; madaraka nchini Saudia sasa yatakuwa yakigawiwa kutoka kwa baba kwenda kwa mwana;  hatua inayohesabiwa kuwa sawa na kumalizika kwa mamlaka ya wana wa Abdulaziz  na kuanza zama mpya za utawala wa watoto wa Salman. Inaonekana kuwa sababu kuu zaidi ya kuongezeka machafuko nchini Saudia inaweza kuhusishwa na mabadiliko hayo muhimu katika safu ya urithi wa madaraka ndani ya utawala huo. 

Khalid al Jayousi ameashiria katika uchambuzi uliochapishwa na gazeti la al Rai al Youm kuhusu ufyatuaji risasi wa mwezi Aprili uliopita karibu na ikulu ya Mfalme wa Saudia na kuandika: Wasaudia walio wengi wanalinasibisha tukio hilo la ufyatuaji risasi katika ikulu ya mfalme huko Riyadh na hitilafu za ndani kati ya viongozi walioko madarakani. Ukweli ni kuwa tunapasa kusema kuwa hata kama wanawafalme wa Saudia kidhahiri wameafiki mabadiliko hayo lakini kushtadi machafuko na ghasia kunaashiria kuwepo hatua na mipango ya kuzusha machafuko kwa lengo la kufelisha jitihada za Muhammad bin Salman za kukalia kiti cha ufalme. 

Nukta ya mwisho ni hii kuwa kuongezeka matukio ya ufyatuaji risasi katika maeneo mbalimbali ya Saudia khususan Riyadh mji mkuu wa nchi hiyo kunadhidhirisha namna serikali ya nchi hiyo inavyokabiliwa na matatizo makubwa katika kudhamini usalama wa ndani; kwa kadiri kwamba si jambo lililo mbali kuwepo uwezekano wa kufanyiwa mabadiliko uongozi wa maafisa usalama nchini humo.  

 

Maoni