• Sababu za njama za Magharibi za kutaka kuvunjwa kikosi cha al Hashdu- Sha'abi nchini Iraq

Laith al Adhari mmoja wa wanachama wa ngazi za juu wa harakati ya kisiasa ya Asaib Ahl al Haq ya Iraq amesema kuwa Marekani inafanya jitihada za kukivunja kikosi cha kujitolea cha wananchi cha Hashdu- Sha'abi na kuitaja hatua hiyo kuwa ni uingiliaji wa wazi wa Washington katika masuala ya ndani ya Iraq.

Kikosi cha Hashdu-Sha'abi kiliundwa mwaka 2014. Kikosi hicho ambacho kina wanachama zaidi ya 100,000 kiliundwa kwa msingi wa kimadhehebu huku lengo lake likiwa ni la kiusalama. Al Hashdu- Sha'abi iliundwa kwa mujibu wa fatwa iliyotolewa na Ayatullah Sistani kiongozi mkubwa wa kidini na marja taqlidi  wa nchini Iraq kwa ajili ya kukabiliana na hujuma za kundi la kigaidi la Daesh.  

Ayatullah Ali as-Sistani, kiongozi mkubwa wa kidini wa Iraq 
 

Swali muhimu ni hili kwamba je, ni kwa nini Marekani na baadhi ya waitifaki wake wa Magharibi wanafanya njama za kukisambaratisha kikosi hicho cha al Hashdu-Sha'abi?  

Jibu muhimu zaidi kwa swali hili ni hili kuwa kikosi cha al Hashdu- Sha'abi si kikosi ambacho kinakwenda sambamba na maslahi ya Marekani kwa upande wa utambulisho na utendaji wake. Katika upande wa utambulisho, Hashdu- Sha'abi ni kundi maalumu linalotambulika miongoni mwa makundi mengineyo nchini Iraq na kiujumla katika Mashariki ya Kati; ambalo linasisitiza kuasisiwa usalama wa ndani na kuwa huru Iraq pasina na uingiliaji wowote wa nchi za Magharibi. Marekani inalitambua kundi kama al Hashu- Sha'abi kuwa linakwenda kinyume na maslahi yake; na imekuwa ikipinga kuimarika makundi ya aina hii katika Mashariki ya Kati. Marekani inatumia nyenzo zake zote dhidi ya harakati kama hizi; ambapo mfano wake ni kuitangaza harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi na wakati huo huo kuiweka chini ya mashinikizo harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen. 

Harakati ya wanamuqawama wa Ansarullah ya Yemen 

Kwa upande wa utendaji, kikosi cha al Hashdu - Sha'abi kimetoa mchango mkubwa na muhimu katika miaka minne ya ushiriki wake katika mchakato wa mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh huko Iraq na kurejesha amani nchini humo na katika maeneo ya mipaka ya nchi hiyo na Syria.  

Jeshi la Iraq mwaka 2014 kwa njia isiyo ya moja kwa moja lilikaribia kusambaratika kwa sababu Mabaathi walikuwa wangali wapo khususan katika safu ya uongozi; na hawakuwa wakiunga mkono wala kufuata mfumo mpya wa kisiasa wa Iraq; ambapo moja ya mifano ya wazi ya hatua hizo ni kukosekana kwa muqawama wa dhati katika kukabiliana na hujuma za Daesh mwaka 2014. Kuundwa kikosi hicho cha kujitolea cha wananchi ambacho wanachama wake walijiunga na kundi hilo kwa hiari yao wenyewe, kulitokana na hatua ya kujilinda. Wanachama wa kundi hilo ni wananchi wa kawaida wa Iraq ambao wameonyesha utiifu wao kwa mfumo mpya wa kisiasa na umoja wa ardhi nzima ya Iraq. Ndio maana Laith al Adhari akakitaja kikosi cha al Hashdu- Sha'abi kuwa mwakilishi wa kisheria wa wananchi wa Iraq kilichojitolea pakubwa katika kukomesha ugaidi nchini Iraq. Utendaji huo pia hauko kwa maslahi ya Marekani kwa sababu Washington inataka yenyewe ndio iongoze suala eti la kurejesha amani huko Iraq na inaamini kuwa 'urejeshaji amani' unaotegemea  vikosi vya ndani si kwa maslahi yake. 

Magaidi wa Daesh 

Suala jingine katika uga wa utendaji wa vikosi hivyo vya kujitolea vya wananchi wa Iraq ni hili kuwa ingawa al Hashdu- Sha'abi imezuiwa kushiriki katika siasa za Iraq, lakini makundi yenye mfungamano na kundi hilo yanashiriki pakubwa katika siasa za Iraq. Aidha orodha ya al Nasr ambayo ilikiunga mkono kikosi cha al Hashdu- Sha'abi katika uchaguzi wa karibuni wa bunge ilishinda vita vingi vya uwakilishi bungeni kwa kuibuka na viti 47 baada ya orodha ya al as-Sairun. Kwa kuendelea kuishinikiza serikali ya Iraq ili ilivunje kundi la al Hashdu- Sha'abi kwa mara nyingine tena Marekani inafanya kila iwezalo kuzuia nafasi muhimu ya kundi hilo katika muundo wa madaraka nchini humo. 

Tags

Jul 12, 2018 04:07 UTC
Maoni