Jul 12, 2018 08:18 UTC
  • Israel yailalamikia Ireland baada ya kupasisha sheria inayopiga marufuku bidhaa zake

Utawala haramu wa Israel umemwita balozi wa Ireland anayeiwakilisha nchi yake katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na kumlalamikia kuhusiana na kupasishwa sheria ambayo inapiga marufuku kuingizwa nchini humo bidhaa zinazotengenezwa katika ardhi hizo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo imedai kwamba kupasishwa kwa sheria hiyo na seneti ya Ireland kutaharibu juhudi za kufanyika mazungumzo eti ya amani kati ya utawala huo wa kibaguzi na  Wapalestina na kwamba kutakuwa na matokeo hasi katika mkondo wa kidiplomasia katika eneo la Mashariki ya Kati. Awali Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ilikuwa imetoa taarifa ikisifu msimamo huo wa Ireland na kuzitaka nchi nyingine zifuate mfano huo wa kijasiri. Kabla ya hapo mswada huo ulikuwa umepitishwa kwa wingi wa kura wa 25-20 ambapo vyama vingi vikubwa viliuunga mkono. Mswada huo ulipendekezwa na Seneta Frances Black ambaye aliwashawishi wabunge wenzake kuunga mkono akisema kuwa Ireland inapasa kuwathibitishia walimwengu kwamba itasimama upande wa kuheshiwa sheria za kimataifa, haki za binadamu na usawa. Amesema katika hali ambayo ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unapingwa na kuchukuliwa na Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na serikali ya Ireland kuwa ni kinyume cha sheria, ni unafiki mkubwa na wa wazi kwa baadhi ya watu kunufaika na biadhaa zinazotokana na uhalifu huo ulio wazi.

Harakati ya kimataifa ya kususia bidhaa zinazotengenezwa Israel

Israel imekuwa ikipanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni tokea iteke ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan mwaka 1967, ambapo jamii ya kimataifa inalitazama jambo hilo na pia udhibiti wake wa ardhi za Wapalestina za mashariki mwa Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa kinyume cha sheria zinazotambulika kimataifa na kusisitiza kuwa eneo hilo linapasa kuwa mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina. Ili kuushinikiza utawala huo uachane na siasa zake hizo za mabavu, ukandamizaji na uporaji wa ardhi za Palestina, nchi nyingi zimepiga marufuku uagizaji wa bidhaa zinazotengenezwa na utawala huo ghasibu.

 

Maoni