Jul 12, 2018 15:01 UTC
  • Amnesty International: Imarati inafanya jinai za kivita Yemen

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa mienendo ya vibaraka wa Imarati dhidi ya mahabusi wanaoshikiliwa katika jela za siri za nchi hiyo huko Yemen ni jinai za kivita.

Ripoti mpya ya Amnesty International imeashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika katika jela za siri za Imarati nchini Yemen na kusema kuwa mienendo hiyo ni jinai na uhalifu wa kivita na kwamba uchunguzi unapaswa kuanza mara moja kuhusu uhalifu huo. 

Ripoti hiyo imesema wapiganaji wanaoungwa mkono na kusaidiwa na Imarati huko Yemen wanawatesa na kuwanyanyasa mahabusi katika jela za siri.

Shirika la habari la Associated Press limefichua kuwa Imarati na washirika wake wana jela 18 za siri huko kusini mwa Yemen na kwamba mahabusi zaidi ya elfu mbili wanateswa na kunyanyaswa kinyama katika jela hizo. 

Shirika la habari la Associated Press limefananisha mbinu za mateso zinazotumiwa na makamanda wa jeshi la Imarati na vibaraka wao kuwatesa raia hao wa Yemen na zile zilizokuwa zikitumiwa na askari wa Marekani katika jela ya kutisha ya Abu Ghuraib nchini Iraq. Limeripoti kuwa, baadhi ya mahabusi wa Yemen wanaoshikiliwa katika jela ya Biir Ahmad wamevuliwa uchi wa mnyama, kulawitiwa na kuteswa maeneo yao ya siri kwa kutumia nyaya za umeme.

Wayemeni wanateswa na kulawitiwa katika jela za siri za Imarati

Vilevile Msemaji wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Elizabeth Trossel amesema kuwa nyaraka na ushahidi uliopo vinaonesha kuwa, askari wa Imarati wanawatesa na kuwadhalilisha kingono mahabusi wa Yemen na kwamba wanaamiliana nao kwa mienendo mibaya. 

Ripoti ya Associated Press inasema: Baadhi ya Wayemen walioteswa kwa kulawitiwa katika jela hizo wamesema kwamba, walitamani kufariki dunia badala ya kukumbana na mateso na udhalilishaji huo mkubwa. Baadhi yao pia wamesema kuwa makamanda wa jeshi la Imarati wanashirikiana na askari wanaosadikiwa kuwa ni Wamarekani na wengine kutoka nchi za America ya Latini.

Maoni