• Kushambuliwa kituo cha kusafisha mafuta Riyadh, hatua mpya katika vita vya Yemen

Ndege ya kivita isiyo na rubani (drone) ya Jeshi la Yemen na Kamati za Kujitolea za Wananchi Wayemen imetekeleza shambulizi ambalo limelenga kwa mafanikio maghala ya mafuta ya kituo cha kusafisha mafuta ya petroli cha Shirika la Aramco la Saudia Arabia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh.

Shirika la Aramco limekiri kuwa kituo chake cha kusafisha mafuta mjini Riyadh kimelengwa na kwamba maghala ya kuhifadhia  mafuta yameteketea.

Ni wazi kuwa ndoto ya Saudia nchini Yemen inazidi kusambaratika na hivyo wakuu wa Riyadh wataambulia patupu katika malengo yao haramu dhidi ya taifa la Yemen. Kinachodhihirika kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ni kuwa,  vita dhidi ya Yemen vimebadilika na kuwa jinamizi kubwa kwa utawala wa kiukoo wa Saudia. Katika miaka ya awali ya vita hivyo, Saudia na waitifaki wake walikuwa ndio tu wenye kutekeleza mashambulizi lakini sasa hali ya vita hivyo imebadilika. Imekuwa jambo la kawaida sasa kusikia Jeshi la Yemen na Kamati za Kujitolea za Wananchi zikiwa zimetekeleza mashambulizi ya makombora  yanaolenga maeneo muhimu na ya kistratijia ndani ya Saudia na hasa katika mji mkuu, Riyadh. Hadi sasa Wayemen wamevurumisha makombora na kulenga kwa mafanikio uwanja wa ndege, kituo cha kijeshi, kasri ya mfalme na kituo cha kusafisha mafuta mjini Riyadh.

Ni wazi kuwa Saudi yenyewe ndio iliyojitumbukiza katika kinamasi nchini Yemen. Saudi ilianzisha vita dhidi ya Yemen lakini sasa haina uwezo wa kumaliza vita hivyo kwani lengo lake katika vita hivyo lilikuwa ni kurejesha kile ilichokuwa ikidai kuwa ni 'uhalali' yaani utawala wa Mansour Hadi, rais aliyestaafu na kutoroka nchi hiyo. Aidha lengo jingine lilikuwa ni  kudhoofisha na hatimaye kuitenga harakati ya Ansarullah ya Yemen.  Mansour Hadi anatazamwa na Wayemen kuwa ni haini na kwa upande wa pili, Ansarullah, kama wanavyokiri weledi wa mambo, ni chombo imara zaidi cha kisiasa Yemen na hivyo haiwezekani kuipuuza harakati hiyo.

Mansour Hadi

Wiki ijayo tutafika katika mwezi wa 40 tokea Saudia ianzishe vita vyakevya kichokozi dhidi ya Yemen. Hujuma ya Jumatano ya  kombora la ndege isiyo na rubani ya vikosi vya nchi hiyo dhidi ya kituo cha kusafisha mafuta katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh ni tukio kubwa na lenye umuhimu katika vita hivyo. Hii ni kwa sababu, kushambuliwa kituo cha Aramco, shirika kubwa zaidi la mafuta duniani, ni jambo ambalo litavuruga uchumi wa Saudi Arabia.

Msemaji wa  Jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Sharaf Qaleb Luqman amesema kushambulia kituo cha Aramco mjini Riyadh kunaashiria kuingia katika hatua mpya vita hivyo ambapo Yemen sasa inaweza kuzuia hujuma ya Wasaudi.

Aidha kushambuliwa kituo hicho cha Aramco kunamaanisha kuwa sasa Saudia haitakuwa tena upande pekee wenye kutekeleza mashambulizi makubwa katika vita hivyo na hivyo inapaswa kusubiri mashambulizi zaidi ya makobora ya Wayemen. Hali kadhalika imethibitika wazi kuwa Saudia haina uwezo wa kujilinda kutokana na makombora ya Wayemen. Kwa maelezo mengine ni kuwa mashmbulizi ya makombora ya Wayemen ni thibitisho kuwa Saudia inaweza kudhuriwa na kupata hasara mwakati wowote. Hii ni katika hali ambayo, baada ya Marekani na China, Saudi Arabia ndio nchi yenye bajeti kubwa zaidi ya kijeshi duniani. Kuhusiana na hilo, gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika: "Pamoja na kuwepo ushirikiano mkubwa wa Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika vita dhidi ya Yemen, lakini  wanajeshi wa Saudi Arabia wameonekana kuwa na mfumo dhaifu."

Wapiganaji wa Kamati za Kujitolea za Wananchi Wayemen 

Inaelekea kuwa, kadiri muda unavyosonga mbele, vita dhidi ya Yemen havitakuwa tena kwa manufaa ya Saudia. Hii ni kwa sababu kipindi cha miezi 40 iliyopita kimeonyesha kuwa, Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen zinazidi kujiimarisha na kupata uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na wavamizi wanaoongozwa na Saudia ambao wanapata himaya ya kigeni. Weledi wa mambo wanasema jeshi la Saudia halina uzoevu wala uwezo wa kivita katika hali ambayo wapiganaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen wanao uzoefu na ujuzi mkubwa wa kivita.

 

Tags

Jul 19, 2018 10:01 UTC
Maoni