• Kutia saini mkataba wa kijeshi na Uhispania; kuendelea siasa za kijeshi za Saudi Arabia

Saudi Arabia imetiliana saini mkataba mpya wa kijeshi na shirika moja la Uhispani ikiwa ni mwendelezo wa mikataba ya kijeshi ya Riyadh na madola ya Magharibi.

Shirika la Viwanda vya Kijeshi la Saudi Arabia (SAMI) Alkhamisi ya juzi lilitiliana saini mkataba na Shirika la Kutengeneza Meli la Uhispani la Navantia kwa ajili ya kununua manowari tano za kivita aina ya Avante 2200.

Saudi Arabia itapatiwa manowari hizo za kivita hadi kufikia mwaka 2022. Moja ya vigezo muhimu kabisa vya Saudi Arabia ni kuwa kwake tegemezi kiusalama kwa madola ya kigeni. Ukweli ni kwamba, mkabala na kudhaminiwa usalama wake na madola ya Magharibi, Saudi Arabia imekuwa ikitumia sehemu kubwa ya pato lake la nishati ya mafuta kwa ajili ya kununua silaha za nchi ambazo kuuza kwake silaha ni sehemu ya pato la nchi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ni kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Saudia imeshika nafasi ya pili duniani kwa kuagiza silaha kutoka nje. Aidha ripoti hiyo inaeleza kwamba, katika kipindi cha miaka hii, kiwango cha Riyadh kununua silaha kimeongezeka kwa asilimia 212.

Silaha zilizotengenezwa Uhispania zimekuwa zikitumiwa na Saudi Arabia kuua watoto huko Yemen

Wakati huo huo, Muhmmad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia hivi karibuni alitangaza kuwa, utawala wa Aal Saud hutumia kiasi cha dola bilioni 70 kila mwaka kwa ajili ya kuingiza nchini humo kutoka nje silaha na zana za kijeshi.

Miongoni mwa nchi za Magharibi, Marekani ni nchi ambayo inapata pato kubwa zaidi kuliko nchi yoyote kutokana na kuiuzia silaha Saudia. Mfano mmoja tu ni mwaka jana pekee wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipofanya safari nchini Saudia alitiliana saini na nchi hiyo mkataba wa kuiuzia silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni 460 ambapo bilioni 110 za mkataba huo zilitekelezwa mara moja huku kiasi cha dola bilioni 350 kilichobakia kitatekelezwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Pamoja na hayo, nchi nyingine za Magharibi kama Uhispania, nayo imekuwa ikiiuzia silaha Saudi Arabia. Wakati wa safari ya Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Aprili mwaka huu huko Uhispania, nchi mbili hizo zilitiliana saini mkataba wa kuiuzia Riyadh manowari za kivita, mkataba ambao ulikuwa na thamani ya takribani dola bilioni 2.2.

Salman bin Abdul Aziz, Mfalme wa Saudi Arabia

Pande mbili zilikubaliana katika mkataba huo kwamba, Shirika la Kutengeneza Manowari za Kivita la Uhispania linalojulikana kama Navantia litaiuzia Riyadh manowari tano za kivita na wanajeshi wa nchi hiyo ya Ulaya kulipatia mafunzo jeshi la Aal saud.

Inaonekana kuwa, mkataba wa Alkhamisi ya juzi baina ya Saudi Arabia na shirika hilo la Uhispania ni katika fremu ya mkataba wa Aprili mwaka huu. Serikali ya Uhispania inatiliana saini mkataba wa kijeshi na Saudi Arabia katika hali ambayo, utawala huo wa Aal Saud umekuwa ukizitumia silaha hizo dhidi ya nchi masikini katika eneo hususan Yemen ambayo ni nchi masikini zaidi miongoni mwa nchi za Kiarabu. Aidha Saudia imekuwa ikiyaunga mkono makundi ya kigaidi hususan katika mgogoro wa Syria.

Hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen iliyoanza Machi 2015 ingali inaendelea ambapo zaidi ya watu 50,000 wameuawa na kujeruhiwa na kuwafanya walimwengu washuhudie maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika miongo ya hivi karibuni.

Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana asasi za kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu hadi sasa zimeitaka mara kadhaa Uhispania na nchi nyingine zinazouunga mkono utawala wa Aal Saudi zisitishe kuiuzia silaha Riyadh. Hata hivyo mkataba wa hivi karibuni kati ya Saudia na Spain unaonyesha kuwa serikali ya Madrid imepuuza matakwa hayo kwa sababu ya dola za mafuta za Saudia huku utawala wa Aal Saud nao ukiendeleza siasa zake za kijeshi.

Tags

Jul 21, 2018 07:04 UTC
Maoni