Jul 26, 2018 03:03 UTC
  • Mashauriano ya Lavrov na Merkel kuhusu Syria

Tangu mwezi Disemba mwaka 2015 Russia ilituma majeshi katika nchi ya Syria kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi na vilevile kuisaidia serikali halali ya nchi hiyo.

Hatua hiyo ya Russia ilifuatia ile ya muungano wa nchi za Kimagharibi na Kiarabu hapo mwaka 2011 wakati zilipoanzisha harakati kubwa ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria na kiongozi wake, Bashar Assad. Hata hivyo harakati hiyo imegonga mwamba na kupata pigo kubwa kutokana na ushindi wa mara kwa mara wa jeshi la taifa la Syria na washirika wake. 

Kwa kutilia maanani umuhimu wa masuala ya Mashariki ya Kati hususan Syria na udharura wa kuwepo mashauriano katika uwanja huo na nchi za Ulaya, Waziri wa Mshauri wa Kigeni wa Russia, Sergei Lavrov Jumanne iliyopita alikutana na kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Ulrike Demmer amesema kuwa, mazungumzo hayo yamejikita zaidi katika hali ya Mashariki ya Kati hususan Syria. Mazungumzo hayo pia yamehudhuriwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani, Heiko Maas na Mkuu wa Majeshi ya Russia, Jenerali Valery Gerasimov. Siku moja kabla yake pia Lavrov na Jenerali Gerasimov walikuwa wamekutana na Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Israel na kuchunguza hali ya Syria. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia ilisema mazungumzo hayo yanafanyika kwa ajili ya kutafuta njia ya utatuzi ya hali ya Syria na jinsi ya kushughulikia wakimbizi wa nchi hiyo. 

Inaonekana kwamba, hali tata ya Syria na kusonga mbele haraka kwa jeshi la nchi hiyo katika mkoa wa Daraa hususan katika maeneo yanayokaribia mpaka wa nchi hiyo na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, kumeutia kiwewe utawala huo ghasibu na kuifanya Ujerumani ilipe mazingatio maalumu suala hilo. Russia inasisitiza udharura wa serikali ya Syria kudhibiti ardhi yote ya nchi hiyo ambayo kwa sasa sehemu yake imevamiwa na makundi ya kigaidi yanayosaidiwa na baadhi ya nchi za Magharibi.

Waziri Mkuu wa Israel na Mfalme Salman wa Saudia

Katika upande wa pili nchi za Magharibi zikiwemo za Ulaya daima zimekuwa zikitatiza suala hilo kwa kutumia visingizio mbalimbali na wakati mwingine vinatumia madai ya kuituhumu serikali ya Syria kuwa imetumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani wake. Mchambuzi wa siasa wa Sweden, Aaron Lund anasema: Katika mtazamo wa kistratijia, Bashar Assad amefanikiwa kuwashinda maadui zake wanaotaka kumuondoa madarakani.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Ujerumani, na Marekani ambayo tangu mwanzoni mwa machafuko ya Syria imekuwa ikifanya jitihada za kudhoofisha serikali halali ya nchi hiyo na kuyaimarisha makundi ya kigaidi, zimeiwekea vikwazo vya aina mbalimbali serikali ya Damascus. Tarehe 28 Mei mwaka huu Umoja wa Ulaya ulirefusha vikwazo vyake dhidi ya Syria kwa mwaka mwingine. Kurefushwa vikwazo hivyo kuna maana ya msimamo usiokuwa mzuri wa umoja huo katika mchakato wa kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa wa Syria. Lengo kuu la nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu lilikuwa kuiondoa madarakani serikali ya Syria na hatimaye kuangamiza kabisa mnyororo wa kambi ya mapambano dhidi ya Wazayuni katika eneo la Mashariki ya Kati. Hata hivyo kuanzisha vita vyenye uharibifu mkubwa huko Syria hakukuwa na faida yoyote kwa muungano huo. Kinyume chake, hivi sasa serikali ya Damascus na washirika wake ndio wanaoshikilia mpini na kudhibiti hali ya mambo.

Marais Bashar Aasad wa Syria, Hassan Rouhani wa Iran na Vladimir Putin wa Russia

Moscow inaunga mkono suala la kuwepo washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria licha ya malalamiko ya mara kwa mara ya maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Magharibi kuhusu suala hilo. Katika hali ya sasa pia makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na kusaidiwa na Marekani na washirika wake, yamedhoofishwa huku serikali ya Syria, ikishirikiana na waitifaki wake yaani Iran, harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Russia ikidumisha mwenendo wa kuyaangamiza makundi hayo na kukomboa maeneo zaidi katika mkoa wa Daraa. Hali hii ni sawa na mwiba katika jicho na koo la utawala haramu wa Israel, Marekani, Saudi Arabia na washirika wao.   

Tags

Maoni