Aug 15, 2018 07:30 UTC
  • Gazeti la Saudia: Mahujaji wa Qatar wachague Hijja au kuuangusha utawala wa nchi yao

Gazeti la Okaz la nchini Saudi Arabia limewataka mahujaji wa Qatar kuchagua moja kati ya mawili, ima kufanya ibada ya Hijja na kuunga mkono utawala wa Al Thani na kwamba iwapo wanataka kutekeleza ibada hiyo, basi wanatakiwa kwanza kuuondoa madarakani utawala huo.

Aidha gazeti hilo limetoa pendekezo kwa utawala wa Aal- Saud kutumia usimamizi wa ibada ya Hijja kama msingi wa kisiasa katika uhusiano wake wa kidiplomasia kwenye mgogoro wa sasa kati yake na Qatar. Kwa mujibu wa wanaharakati wa masuala ya kisheria, Saudia inaitumia ibada ya Hijja kwa ajili ya kufikia malengo yake ya kisiasa na kwamba suala hilo linakiuka sheria za kimataifa na haki za binaadamu. Wakati huo huo, Sheikh Ahmed al-Raysouni, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Maulama wa Waislamu amezungumzia mwenendo wa utumiwaji wa ibada ya Hijja katika masuala ya kisiasa kunakofanywa na Saudia kwa kusema, Riyadh inawazuia Waislamu wa Qatar, Canada, na wapinzani wengine kutekeleza ibada ya HIjja.

Ibada ya Hijja

Kwa mujibu wa Sheikh Ahmed al-Raysouni, Saudia inatakiwa iachane na usimamizi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu  na badala yake usimamizi wa ibada hiyo uchukuliwe na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kama mwakilishi wa Waislamu walio wengi duniani. Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zilitangaza kukata mahusiano yao na Qatar, tarehe tano Juni mwaka jana, baada ya serikali ya Doha kukataa kuwa chini ya satua ya Riyadh. Mbali na kukata mahusiano yao, nchi hizo ziliiwekea Qatar mzingiro wa ardhini, angani na baharini.

Tags

Maoni