Aug 17, 2018 02:35 UTC
  • Ujumbe wa majaribio ya makombora ya Hamas baharini kwa Israel na waitifaki wake

Mtandao wa habari wa Moa umezinukuu duru za Kizayuni na kutangaza kuwa brigedi za Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika wiki za karibuni zilivurumisha makombora kuelekea baharini; hatua ambayo imetekelezwa katika fremu ya kufanyia majaribio uwezo wa kijeshi wa wanamapambano wa Palestina.

Mapigano kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) yamepamba moto katika miezi ya hivi karibuni. Zaidi ya yote, hatua na siasa zinazotekelezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, zimeandaa mazingira ya kushtadi mapigano kati ya harakati Hamas na Israel. Mwezi Disemba mwaka jana Trump aliutangaza rasmi mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kuwa eti mji mkuu wa Israel badala ya Tel Aviv; na mwezi Mei mwaka huu pia akauhamishia huko Quds ubalozi wa Marekani. Mbali na hilo, serikali ya Marekani ina nia ya kutekeleza mpango ujulikanao kwa jina la "Muamala wa Karne" kwa lengo eti la kutatua mvutano kati ya Israel na Palestina. Hata hivyo mpango huo upo kwa ajli ya kuhudumia maslahi ya utawala wa Israel. Hatua zote hizi zinazochukuliwa na serikali ya Trump zimeufanya utawala wa Kizayuni wa Israel uzidishe zaidi jinai zake dhidi ya raia wa Palestina hususan wakazi wa Ukanda wa Ghaza.  

Wapalestina katika maandamano ya kila Ijumaa ya Haki ya Kurejea huko Ukanda wa Ghaza

Wananchi wa Palestina pia wamechagua stratejia ya muqawama katika kukabiliana jinai hizo za utawala wa Israel. Stratejia hiyo ya muqawama inatekelezwa katika kalibu ya kufanyika maandamano ya "Haki ya Kurejea" na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na chokochoko za Wazayuni. Maandamano ya kurejea ambayo yalianza Machi 30 yangali yanaendelea hadi hivi sasa. Wananchi wa Palestina wanaendeleza mapambano yao dhidi ya Maghasibu wa Kizayuni licha ya kuuliwa shahidi karibu Wapalestina 160 na kujeruhiwa wengine zaidi ya elfu 17. Hii ni kwa sababu wananchi hao wanatambua vyema kwamba kutekelezwa mpango huo wa Muamala wa Karne kunamaanisha kuwaondoa raia hao katika historia, jiografia na utambulisho wao wa asili na kuwafuta katika ardhi ya Palestina. 

Muqawama wa Palestina nao unaendelezwa katika kalibu ya kuimarisha uwezo wa kujlinda na kukabiliana na mashambulizi ya Israel licha ya kufanyika maandano ya haki ya kurejea. Majaribio ya makombora ya baharini ya harakati ya Hamas bila ya shaka yamefanywa katika fremu hiyo hiyo ya kuongeza nguvu ya kujilinda ya kambi ya muqawama mbele ya utawala wa Kizayuni.

Wamamuqawama wa brigedi ya Izzuddin Qassam wakijiandaa kuvurumisha makombora yao

Kigezo cha kuimarisha uwezo wa kujilinda kilichodhihirishwa na Hamas kimetokana na tajiriba ya historia iliyoipata harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon katika vita vya siku 33 mwaka 2006; vita ambavyo vilitoa pigo la kihistoria kwa utawala wa Israel kutokana na  nguvu ya kujilinda iliyokuwa nayo Hizbullah. Ujumbe wa brigedi za Izzuddin Qassam uliochapishwa Jumamosi iliyopita katika tovuti ya habari ya vikosi hivyo ulibainisha kuwa: Jaribio la adui Mzayuni la kuchukua hatua yoyote ya kifedhuli litakuwa angamizo na litausabababishia utawala huo madhara yasiyoweza kustahimilika ambayo haujawahi kuyashuhudia iwe katika asili au ukubwa wake.   

Majaribio ya makombora ya brigedi za al Qassam yamebeba pia ujumbe maalumu kwa Israel kwamba Wapalestina kivyovyote vile hawataruhusu kutekelezwa mpango huo wa Muamala wa Karne hata kama utawala huo na waitifaki wake watatenda jinai ya kihistoria dhidi ya Wapalestina kwa kuwafungia raia hao vivuko vyote. Inaonekana kuwa ujumbe huo umepokewa pia na serikali ya Trump, na baadhi ya nchi za eneo hili mbali na utawala za Kizayuni kwa sababu Marekani imetangaza kuakhirisha mpango huo wa Muamala wa Karne, huku Saudi Arabia ikilegeza msimamo katika kuunga mkono mpango huo na utawala wa Kizayuni ukilazimika kukifungua kivuko cha Karam Abu Salim kutokana na mashinikizo ya fikra za walio wengi.  

Maoni