Aug 17, 2018 14:18 UTC
  • Kukataa Bahrain wito wa UN wa kuwaachia huru wanaharakati wa haki za binadamu

Utawala wa Bahrain umekataa wito wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa kumwachilia huru Nabil Rajab, mtetezi wa haki za binadamu anayeshikiliwa kwenye jela za utawala huo.

Wataalamu kadhaa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu wametangaza kuwa kuwekwa kizuizini Nabil Rajab ni kinyume cha sheria na ni ukiukaji wa uhuru wa kutoa maoni. Jana Alkhamisi, utawala wa Aal Khalifa ulitoa taarifa ya kupinga maelezo ya jopo la wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa kwamba utawala huo umewatia nguvuni kiuonevu wanaharakati wa masuala ya sheria na haki za binadamu akiwemo Nabil Rajab na ukadai kwamba makosa waliyofanya wanaharakati hao hayana uhusiano wowote na mitazamo yao ya kisiasa. Karibu miaka mitatu iliyopita maafisa usalama wa utawala wa Aal Khalifa walimtia nguvuni Nabil Rajab akiwa nyumbani kwake na kuvishikilia vitu vyake kadhaa vya binafsi ikiwemo kompyuta yake ya mkononi. Mashtaka yanayomkabili mwanaharakati huyo wa haki za binadamu ni mahojiano ya televisheni aliyofanyiwa mwaka 2015 na 2016 ambapo kwa mujibu wa maafisa wa utawala wa Aal Khalifa, katika mahojiano hayo Nabil Rajab alilitia doa jina na sura ya nchi hiyo. Utawala wa Bahrain unatumia kila tuhuma chafu na wenzo wowote ule wa kionevu ili kuwaandama wanaharakati wa kisiasa na kisheria ambao wanapigania haki za kisheria za raia wa Bahrain na kutaka kuwepo utawala unaotokana na ridhaa ya wananchi wa nchi hiyo.

Nabil Rajab

Tangu  tarehe 14 Februari mwaka 2011 Bahrain imekuwa uwanja wa mapinduzi ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa. Lakini jibu la utawala huo limekuwa ni kuwatia nguvuni wananachi wanaoandamana na pia viongozi wa upinzani kisha kuwafungulia kesi bandia na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela.

Jumuiya ya Al-Wifaq nchini Bahrain imetangaza kuwa tangu mwaka 2011 hadi sasa, wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano yapatayo elfu hamsini, ya kutaka kuwepo nchini mwao utawala unaotokana na ridhaa yao wenyewe. Sheikh Hussein Ad-Dayhi, Naibu Mkuu wa jumuiya hiyo ya Kiislamu amebainisha hayo na kuongeza kwamba maandamano hayo yamefanyika licha ya kupigwa marufuku mikusanyiko sambamba na kukandamizwa maandamano ya amani yanayofanywa na wananchi. Sheikh Ad-Dayhi amefafanua kwamba baada ya miaka kadhaa ya kuyakandamiza maandamano ya amani, mnamo mwezi Desemba mwaka 2014 utawala wa Aal Khalifa ulipiga marufuku kikamilifu mikusanyiko ya aina yoyote ile ya watu; lakini pamoja na hayo Bahrain ingali ni uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga serikali.

Maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain kutaka Nabil Rajab aachiwe huru

Katika kipindi chote hicho, kwa msaada wa vikosi vya jeshi vilivyotumwa kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, utawala wa Aal Khalifa umeendelea kutumia mkono wa chuma kukanadamiza maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain ambapo hadi sasa umeshaua makumi ya waandamanaji na kuwatia jela maelfu ya wapinzani wakiwemo wanaharakati wa kisiasa na kisheria.

Sheikh Murtadha As-Sanadi, kiongozi wa harakati ya Al-Wafaul-Islamiy amesema, utawala wa Aal Khalifa unawakomoa kisiasa wanamapinduzi wa Bahrain na kubainisha kuwa hadi sasa zaidi wanaharakati 200 wameuawa kutokana na utumiaji nguvu na mabavu wa watawala wa nchi hiyo dhidi ya wapinzani.

Sera za utumiaji mkono wa chuma za utawala wa Bahrain hazijawa na matokeo mengine isipokuwa kuendelea mauaji ya wapinzani na kufurika jela za utawala huo wanaharakati wa kisiasa na wa haki za binadamu. Kwa kushadidisha hatua za kipolisi na utumiaji mabavu, kuwawekea vizuizi vikali wanaharakati wa kisiasa na wa haki za binadamu, kuwatia nguvuni, kuwazushia tuhuma zisizo na msingi na hata kwa kuwanyonga wafungwa wa kisiasa, utawala wa Aal Khalifa umefunga njia zote za mazungumzo ya kisiasa na kuielekeza Bahrain kwenye anga ya udikteta wa kisiasa na kipolisi. Kushamiri maandamano ya upinzani nchini Bahrain na ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa kumewafanya walimwengu wazidi kuguswa na matukio yanayojiri nchini humo; na ni hali hiyo ndiyo iliyoibua wasiwasi wa wataalamu wa masuala ya sheria na haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.../

Tags

Maoni