Aug 22, 2018 03:41 UTC
  • OIC yasisitiza kuhifadhiwa hali ya kihistoria ya Masjidul al-Aqswa

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imesisitiza juu ya udharura wa kulindwa na kuhifadhiwa hali ya kihistoria ya Msikiti wa al-Aqswa licha ya kuendelea hujuma, uvamizi na jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya msikiti huo mtakatifu.

Sisitizo la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) limetolewa katika taarifa ya jumuiya hiyo iliyotolewa jana kwa mnasaba wa mwaka wa 49 tangu Msikiti wa al-Aqswa ulipochomwa moto na kueleza kwamba, Israel imekuwa ikiendeleza siasa zake za kuuyahudisha mji wa Beitul-Muqaddas.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesisitiza kuwa, hatua za Israel dhidi ya mji wa Beitul-Muqaddas na hususan Msikiti wa al-Aqswa zinakinzana na sheria pamoja na maazimio ya kimataifa.

Msikiti wa al Aqsa ulichomwa moto na Wazayuni wa Israel

Aidha OIC imesisitiza juu ya haki ya Wapalestina ya kuurejesha mji wa Quds katika mamlaka yao na kulinda maeneo yote ambayo ni matukufu ya Uislamu na Ukristo katika mji huo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeitaka pia jamii ya kimataifa kuushinikiza utawala vamizi wa Israel ili uheshimu sheria na maazimio ya kimataifa na hivyo uhitimishe uvamizi na ukaliaji wake mabavu wa ardhi za Palestina.

Jana tarehe 21 Agosti ilisadifiana na siku Msikiti wa al-Aqswa ulipochomwa moto na Wazayuni. Israel ilidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Baada ya tukio hilo nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ambayo leo inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Tags

Maoni