Aug 26, 2018 14:53 UTC
  • Idara ya Waqfu ya Baitul Muqaddas: Msikiti wa Al-Aqsa ni sehemu ya itikadi ya kila Muislamu

Idara ya Waqfu ya Quds na masuala ya msikiti wa Al-Aqsa imesisitiza kuwa msikiti huo mtukufu ni sehemu ya asili ya itikadi ya kila Muislamu na kwa hivyo hauwezi kugawanywa wala kuwashirikisha watu wengine.

Taarifa iliyotolewa na Idara hiyo imeeleza kuwa, mahakama ya utawala wa Kizayuni wa Israel haina haki ya kutoa hukumu yoyote kuhusu msikiti wa Al-Aqsa na kwamba msikiti wa Al-Aqsa utaendelea kubaki kuwa msikiti wa Waislamu pekee na wala hakuna mtu yeyote aliye mshirika kwenye msikiti huo.

Idara ya Waqfu ya Quds na masuala ya msikiti wa Al-Aqsa imebainisha kuwa kupitisha uamuzi wa kutekelezwa ibada ya aina yoyote kwa wasio Waislamu ndani ya msikiti wa Al-Aqsa na kubadilisha hali ya kihistoria, kidini na kisheria ya msikiti huo ya kipindi cha kabla na baada ya mwaka 1967 ni uchokozi wa dhahiri dhidi ya Uislamu na Waislamu wa ulimwengu mzima.

Walowezi wa Kizayuni wakisindikizwa na askari wa Israel wakiwa ndani ya eneo la msikiti wa Al-Aqsa baada ya kuuvamia msikiti huo

Taasisi hiyo imetahadharisha juu ya kuchukuliwa uamuzi wowote utakaosababisha kubomolewa na kufutwa athari za msikiti wa Al-Aqsa na vilevile kuhusu athari hasi za hatua za makundi ya Kizayuni yenye misimamo ya kufurutu mpaka yanayojaribu kuchochea moto wa vita vya kidini katika Mashariki ya Kati, ambao kwa msaada na uungaji mkono wa wanajeshi wa Kizayuni na wanasiasa wa utawala huo wameshafanya na wanaendelea kufanya jinai kadha wa kadha dhidi ya kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.

Katika kile kinachotajwa kuwa jaribio la kulifanya kuwa sheria suala la ufanyaji ibada wa wasio Waislamu, Mahakama Kuu ya utawala haramu wa Israel imelipa baraza la mawaziri la utawala huo wa Kizayuni muda wa siku 60 litoe sababu za kupiga marufuku Mayahudi wasitekeleze ibada zao ndani ya msikiti wa Al-Aqsa.

Mwaka 2003, utawala wa Kizayuni ulitoa idhini kwa walowezi wa Kizayuni ya kuingia ndani ya msikiti wa Al-Aqsa; na kuanzia mwaka huo hadi sasa Wazyuni wamekuwa kila mara wakiuvamia na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu.../

Tags

Maoni