Aug 27, 2018 07:32 UTC
  • Indhari ya Wapalestina kuhusu kugawanywa msikiti wa al Aqsa

Idara ya Waqfu ya Quds na inayosimamia msikiti wa al Aqsa imesisitiza kuwa msikiti huo ni sehemu takatifu kiimani na kiitikadi ya kila Muislamu isiyoweza kugawanywa wala kuwa na ubia.

Idara hiyo ya Waqfu na inayosimamia msikiti wa al Aqsa imesema kuwa kitendo cha kuwaidhinishia watu wasio Waislamu kufanya sala na ibada zozote katika msikiti wa al Aqsa na kubadilisha hali ya kihistoria, kidini na kisheria ya msikiti huo ni uchokozi wa waziwazi dhidi ya Uislamu na Waislamu kote ulimwenguni. Duru mpya ya harakati na chokochoko za utawala wa Kizayuni kwa shabaha ya kuyakalia kwa mabavu hatua kwa hatua  maeneo ya Palestina khususan maeneo matakatifu ukiwemo msikiti wa al Aqsa imekabiliwa na radiamali kubwa za fikra za waliowengi duniani. Israel imekusudia kuugawa msikiti huo kwa kubadili utambulisho wake wa Kiislamu na kisha kufuta mamlaka ya wakfu wa Kiislamu unaosimamia msikiti huo mtakatifu. Kwa mujibu wa miswada miwili muhimu na ya kihistoria ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; maazimio nambari 338 na 242 ya baraza hilo yanaitambua Baitul Muqaddas kuwa ni eneo linalokaliwa kwa mabavu; na utawala wa Kizayuni unapasa pia kuondoka eneo hilo bila ya sharti lolote kwa kuzingatia kuwa hauna haki yoyote ya kuvamia na kuukalia kwa mabavu mji huo pamoja na athari zake za kihistoria kama msikiti wa al Aqsa. Kuendelea uvamizi na vitendo vya kujitanua vya utawala wa Kizayuni katika msikiti wa al Aqsa si tu kuwa kunakiuka sheria na taratibu za kimataifa bali ni kinyume pia na matamko ya utawala huo mkabala na Wapalestina na nchi za Kiarabu.  

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1994 kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Jordan, ni marufuku kufanyika ibada za Wazayuni katika eneo la uwanja wa msikiti wa al Aqsa. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) pia liliwasilisha hoja na kupinga kuwepo uhusiano wowote wa kihistoria, kidini au wa kiutamaduni kati ya Wayahudi na maeneo matakatifu huko Quds khususan msikiti wa al Aqsa; na kuutaja msikiti huo kuwa eneo takatifu la Waislamu. Matukio ya Palestina yanaonyesha kuwa maghasibu wa Kizayuni wanatekeleza marhala ya mwisho ya njama zao za kuudhibiti msikiti wa al Aqsa. Ni wazi kuwa utawala huo umedhamiria kuimarisha udhibiti wake wa mabavu dhidi ya Wapalestina kwa kutumia mbinu mbalimbali, kukiwemo kuwazuia Wapalestina kufika katika maeneo ya Palestina na yale matakatifu ya Kiislamu. Ushahidi unaonyesha kuwa kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani na hatua yake ya kutoa mkono wa baraka kwa hatua za kijuba na kupenda kujitanua za Israel katika maeneo ya Palestina khususan huko Quds, kumedizidisha njama za utawala huo haramu katika maeneo mbalimbali ya Palestina  ikiwemo Baitul Muqaddas. 

Rais Donald Trump wa Marekani 

Katibu Mkuu wa Kamati ya Utekelezaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina amesisitiza kuwa serikali ya sasa ya Marekani imepuuza kadhia ya Palestina na inataka kuikabidhi kikamilifu Quds kwa utawala wa Kizayuni. Akizungumza katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al Mayadin ya Lebanon, Swaib Uraiqat amesema kuwa Wapalestina hawataacha haki yao ya kuendesha mapambano  kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kwamba amani haitapatikana iwapo serikali ya Palestina haitatambuliwa rasmi huku mji wake wake mkuu ukiwa ni Quds.  

Swaib Uraiqat, Katibu Mkuu wa kamati ya utekelezaji ya harakati ya Ukombozi wa Palestina 

 

       

Tags

Maoni