Sep 07, 2018 07:20 UTC
  • Mkutano wa Troika ya Syria mjini Tehran, kigezo bora cha kuigwa cha uishirikiano wa kikanda

Leo Ijumaa Tehran ni mwenyeji wa kikao cha viongozi wa nchi tatu muhimu katika mchakato wa kurejesha amani nchini Syria, yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki.

Marais wa Iran, Russia na Uturuki wanakutana leo mjini Tehran kuchunguza hali ya Syria wakati nchi hiyo ikipiga hatua za mwisho za kupambana na ugaidi, huku mgogoro wa nchi hiyo ukielekea zaidi katika awamu ya masuala ya kisiasa. Kwa sasa eneo la Idlib pekee ndilo linalodhibitiwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi na waitifaki wao wa Kiarabu. 

Mafanikio ya jeshi la Syria katika vita dhidi ya magaidi sambamba na mchakato wa kisiasa nchini humo ni matokeo ya ushirikiano wa Iran, Russia na Uturuki chini ya mwavuli wa mazungumzo ya amani ya Astana. Hii leo Marais Hassan Rouhani wa Iran, Vladimir Putin wa Russia an Recep Tayyep Erdogan wanakutana mjini Tehran huku vita vya Syria vikielekea ukingoni na juhudi kubwa zaidi zikielekezwa katika operesheni ya kukomboa eneo la Idlib. Tangazo la kumalizwa kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria na kusafishwa maeneo yote ya Syria ni kielelezo cha umuhimu wa Troika ya Syria ambayo viongozi wake wanakutana leo mjini Tehran kujadiliana na kushauriana juu ya mustakbali wa Syria ya baada ya vita.

Jeshi la Syria limefanikiwa kuangamzia makundi mengi ya kigaidi.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, sasa Syria imeondoka katika awamu ya mapigano ya kijeshi na inaelekea katika mchakato wa kisiasa. Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi anasema: "Mchakato wa mazungumzo ya Astana yanayosimamiwa na Iran, Russia na Uturuki umekuwa na mafanikio makubwa katika kupambana na ugaidi na kupungua mivutano." Araqchi ameongeza kuwa, magaidi wameangamizwa katika maeneo mengi ya Syria na kwamba waliosalia wamekimbilia katika mkoa wa Idlib. 

Abbas Araqchi

Ushindi wa jeshi la Syria na waitifaki wake umekuwa na taathira kubwa kiasi cha kuzitia kiwewe na kihoro nchi zinazoyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini humo. Ushindi huo unasaidiwa na ushirikiano wa Iran, Russia na Uturuki ambao sasa unatambuliwa kuwa kigezo bora cha kuigwa katika masuala ya ushurikiano wa kikanda na kimataifa. 

Kwa kutilia maanani hali ya sasa ya Syria inajulikana wazi kuwa ushirikiano wa troika unaoielekeza Syria katika upande wa kuyaangamia kikamilifu makundi ya kigaidi ndio ushirikiano bora ambao viongozi wake wanakutana leo mjini Tehran licha ya makelele mengi ya kipropaganda ya nchi za Magharibi ili kupiga hatua za mwisho za kupambana na magaidi katika eneo la Idlib na kuchukua maamuzi muhimu kuhusu mustakbali wa kisiasa wa Syria.    

Tags

Maoni