Sep 07, 2018 13:47 UTC
  • Majibu makali ya kijeshi ya Yemen kwa tabia ya kupenda vita ya ukoo wa Aal Saud

Kitendo cha ukoo wa Aal Saud unaotawala kidikteta nchini Saudi Arabia, cha kufunga njia zote za kupatikana utatuzi wa kisiasa na wa amani wa mgogoro wa Yemen sambamba na kuendelea na jinai zake nchini humo, kimepata majibu makali ya muqawama wa wananchi wa Yemen.

Athari mbaya za hatua za hivi karibu kabisa za ukoo wa Aal Saud za kukwamisha utatuzi wa mgogoro wa Yemen, ni ukwamishaji wa Riyadh uliopelekea kuakhirishwa mazungumzo ya Geneva. 

Sababu kuu iliyopelekea kuakhirishwa mazungumzo hayo ni ukwamishaji wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kwani pamoja na kwamba Baraza Kuu la Kisiasa la harakati ya Answarullah lilikuwa limekubali kutuma ujumbe wake huko Geneva, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia umeizuia ndege ambayo ilikuwa itokee Oman na kutua katika uwanja wa ndege wa Sana'a kwa ajili ya kuuchukua ujumbe huyo wa Answarullah na kuupeleka Geneva Uswisi kushiriki katika mazungumzo hayo. Hii si mara ya kwanza kwa muungano vamizi wa Saudia kutumia mbinu kama hiyo kukwamisha mazungumzo ya amani ya Yemen. Hatua hiyo ya Saudi Arabia imechukuliwa katika hali ambayo nchi hiyo na wavamizi wenzake wameongeza mashambulio yao dhidi ya watoto wadogo na wanawake wa Yemen katika miezi ya hivi karibuni.

Shirika la taifa la mafuta la Saudia, ARAMCO

 

Kikijibu jinai hizo za Saudia, kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen na kamati za wananchi za nchi hiyo zimetangaza habari ya kuushambulia uwanja wa ndege wa Jizan wa Saudi Arabia kwa makombora mawili ya belestiki aina ya Badr-1 yaliyotengenezwa ndani ya Yemen. Kikosi cha makombora cha jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen hivi karibuni pia zilishambulia shirika la taifa la mafuta la Saudia ARAMCO pamoja na kiwanda cha petrokemikali cha Jizan kwa kutumia makombora ya balestiki ya Badr-1. Kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo zinafanya mashambulizi ya makombora takriban kila siku kupiga maeneo muhimu ndani ya ardhi ya Saudia ikiwa ni kujibu jinai za kila leo zinazofanywa na nchi vamizi za kushambulia raia wa Yemen. 

Vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vinategemea uwezo wao wa ndani wa kutengeneza makombora ya masafa tofauti kujibu mashambulio ya Saudi Arabia na wavamizi wenzake tangu wavamizi hao walipoivamia nchi hiyo karibu miaka minne sasa. Stratijia hiyo ya kujibu jinai za wavamizi kwa kutumia makombora imelisaidia sana jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen kiasi kwamba wavamizi wa nchi hiyo ya Kiarabu ambao walikuwa na tamaa ya kumaliza vita hivyo katika kipindi kifupi tu, sasa hivi wamekwama kwenye kinamasi ambacho ni vigumu na ni fedheha kutoka. Licha ya Saudia na wavamizi wenzake kufanya jinai kubwa dhidi ya raia na kushambulia kila kitu huko Yemen, lakini kila leo wananchi wanamuqawama wa nchi hiyo ya Kiislamu wanazidi kuwa na imani imara ya kujilinda na ndivyo jeshi lao na vikosi vya kujitolea vya wananchi vinavyozidi kushambulia maeneo ya ndani zaidi ya madola vamizi kama Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Amma jinai za wavamizi wa Yemen dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu zinaendelea huku mashirika ya kimataifa yakishindwa kuchukua hatua yoyote ya maana ya kuwalazimisha wavamizi hao kukomesha jinai zao nchini Yemen.

Kombora la balestiki la Badr1 la Yemen

 

Mohammad Ali al Houthi, mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen, sambamba na kulaani mashambulizi ya muungano wa Saudia nchini Yemen amesema, mashirika na vyombo vya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa vimechukua misimamo dhaifu mbele ya jinai za Saudi Arabia nchini Yemen, na hivyo kupoteza hata ile sehemu ndogo ya heshima viliyokuwa nayo.

Amma jambo la kutia moyo ni muqawama wa wananchi wa Yemen ambao wamethibitisha kivitendo kuwa, kamwe hawako tayari kuwaruhusu wavamizi wa nchi yao kufikia malengo yao haramu na hii ina maana kuwa wananchi hao wataendelea kuwa pamoja na jeshi na vikosi vya kujitolea vya Answarullah, suala ambalo lenyewe kwa udhati wake ni pigo kubwa kwa wavamizi wa Yemen ambao lengo lao hasa ni kuisambaratisha harakati ya Kiislamu ya Answarullah.

Maoni