Sep 08, 2018 06:57 UTC
  • Mkutano wa pande tatu Tehran; azma ya kweli ya kuangamiza ugaidi katika mji wa Idlib Syria

Mkutano wa Marais wa Iran, Russia na Uturuki umefanyika hapa mjini Tehran ajenda kuu ikiwa ni matukio ya Syria.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba muhimu katika mkutano huo kuhusiana na matukio ya Syria pamoja na vita dhidi ya ugaidi katika mji wa Idlib. Akihutubia alasiri ya jana Ijumaa katika mkutano wa pande tatu mjini Tehran uliohudhuriwa na Marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki, Rais Rouhani sambamba na kubainisha kwamba, utatuzi wa kijeshi wa mgogoro wa si mtutu wa bunduki ameeleza kwamba: Vita dhidi ya ugaidi katika mji wa Idlib ni sehemu ya majukumu yasiyoepukika ya kurejesha amani na uthabiti nchini Syria; hata hivyo vita hii haipasi kuwadhuru raia.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, hakuna mpango wowote wa kupambana na ugaidi ambao unaweza kufanikiwa bila ya kuzingatia chimbuko la kuibuka kwa ugaidi. Waanzilishi na wasababishaji wa ukaliaji mabavu, ugaidi, uvamizi, uingiliaji wa kigeni na ubaguzi kama Marekani, utawala ghasibu wa Israel na baadhi ya waungaji mkono wa ugaidi, hawawezi kubadilisha nafasi yao ya 'mtuhumiwa' na kuwa ya 'mtoa tuhuma' kwa kutumia njia za propaganda, domokaya na makelele.

Mkutano wa pande tatu za Iran, Russia na Uturuki - Tehran (07.09.2018)

Mkutano wa Tehran kuhusu Syria na mambo yaliyogusiwa katika hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ishara ya kuwa wa haki mhimili wa mapambano dhidi ya ugaidi ambapo viongozi wa mhimili huo wamekutana hapa Tehran katika moja ya vipindi na mazingira nyeti kabisa.

Russia, Uturuki pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao ndio wabunifu wa mchakato wa "mazungumzo ya Astana" zimekuwa na nafasi muhimu na athirifu katika mchakato wa kisiasa na vita dhidi ya ugaidi nchini Syria, na hii leo matukio ya kimedani ya nchi hiyo yanaonyesha juu ya kufanikiwa mwenendo huu wenye taathira chanya katika Mashariki ya Kati. Nchi wanachama wa mchakato wa Astana ambazo zinafanya mambo kinyume na irada na matakwa ya Marekani ndio watoaji wa madai ya kweli ya kupambana na ugaidi. Hapana shaka kuwa, madai yao yameonekana kuwa ni ya kweli na ya haki hasa kutokana na kuzidi kubanwa uwepo wa magaidi katika mji wa Idlib.

Katika mazingira kama haya, waungaji mkono wa ugaidi ikiwemo Marekani na Israel zimekuwa zikizusha makele yasiyo na maana zikitaka kuendelea kuwepo magaidi huko Syria.

Mazungumzo ya Marais Hassan Rouhani wa Iran na Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa mkutano wa pande tatu

Katika siku za hivi karibuni, utawala haramu wa Israel na Marekani pamoja na washirika wao wenye nafasi haribifu katika matukio ya Syria, wameanzisha vita vya kisaikolojia kwa kile wanachodai kwamba, eti kuwaunga mkono wananchi wa Syria, ili kwa njia hiyo waweze kuzuia operesheni ya kukombolewa mji wa Idlib.

Katika uwanja huo, ndege za kivita za Israel Jumanne iliyopita zilifanya mashambulio kadhaa katika mkoa wa Hama nchini Syria. Sambamba na mashambulio hayo, kundi linalojulikana kama 'Watu wa Kofia Nyeupe" wakiungwa mkono na  mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza walikuwa wakifanya mazoezi kando kando ya mji wa Idlib wakiwa na lengo la kuendeleza senario ya kutekeleza shambulio la silaha za kemikali linaloratibiwa  ili operesheni ya kijeshi dhidi ya Idlib itakapoanza walituhumu jeshi la Syria kwamba, limetumia silaha za kemikali.

Senario kama hii imewahi kufanyika hapo kabla nchini Syria, ambapo mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, Marekani, Uingereza na Ufaransa zikitumia madai hayo ya kutumia jeshi la Syria silaha za kemikali katika mji wa Ghouta Mashariki, zilifanya mashambulio ya pamoja ya makombora katika viunga vya mji mkuu Damascus. Mashambulio hayo pamoja na malengo yaliyokusudiwa ni mambo yanayoonyesha kwamba, Marekani na washirika wake nchini Syria si sehemu ya njia za ufumbuzi bali ni sehemu ya matatizo na mgogoro wa nchi hiyo na wamekuwa wakicheza mpira katika uwanja wa magaidi.

Mazungumzo ya Marais Hassan Rouhani wa Iran (kulia) na Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki

Stephan Landsman mwandishi na mnadharia wa Kimarekani ameandika: Wale wanaojulikana kama waasi au makundi ya upinzani ya serikali ya Syria, ndio wale mamluki walioajiriwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) na lile la Israel MOSSAD ili wahudumie tamaa na matakwa haramu ya Washington, NATO, Israel, na tawala za Mashariki ya Kati ambazo zinapinga nchi ya Syria kuwa na mamlaka yake ya kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Kwa kuzingatia ukweli huu, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema alasiri ya jana katika mkutano wa pande tatu mjini Tehran kwamba: Uingiliaji wa Marekani usio wa kisheria katika masuala ya ndani ya Syria hauoani na kanuni yoyote ile ya kimataifa, bali unaiongezea matatizo nchi hiyo ya Kiarabu na kuufanya mwenendo wa kupatikana amani ya kudumu nchini Syria ukabiliwe na changamoto kubwa.

Katika fremu hiyo hiyo, taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano wa pande tatu wa Marais wa Iran, Uturuki na Russia hapa mjini Tehran hapo jana, ilitilia mkazo juu ya kuhifadhiwa ardhi yote ya Syria pamoja na mamlaka yake na kuelezwa kinagaubaga kwamba: Mgogoro wa Syria katu hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Tags

Maoni