Sep 09, 2018 02:20 UTC
  • Chanzo na taathira za machafuko huko Basra

Machafuko katika mkoa wa Basra kusini mwa Iraq yamepamba moto tangu Jumanne iliyopita tarehe 4 Septemba na hadi kufikia sasa watu 11 wameuliwa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Baada ya kushtadi ghasia na machafuko huko katika mkoa wa Basra kamandi ya oparesheni za pamoja nchini Iraq ameyataja matukio hayo kuwa ya kichochezi na kuwaamuru askari usalama kukabiliana vikali na wafanyafujo na maandamano ya kichochezi mkoani humo. Wakati huo huo imeelezwa kuwa askari usalama kadhaa kutoka Baghdad wameelekea mkoani Basra. 

Swali muhimu linaloulizwa ni hili kuwa je, nini chanzo cha machafuko hayo huko Basra? Tunaweza kutoa majibu mawili kuhusiana na ghasia hizo. Jibu la kwanza ni kwamba maandamano mkoani Basra yamesababishwa na kuwepo udhaifu mkubwa katika utolewaji wa huduma za kijamii. Wakazi wa mkoa huo wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kimaisha yakiwemo matatizo ya upatikanaji maji na umeme na vile vile kuwepo kiwango kikubwa cha watu wasio na ajira. Kwa kutegemea takwimu zilizopo mahospitalini, Kamisheni ya Haki za Binadamu imetangaza kuwa wakazi elfu 20 wa Basra wamedhurika kutokana na kuchafuka maji. Wafanya maandamano mkoani humo wanaamini kuwa hali waliyonayo haiendani na hadhi ya mkoa huo ambao unajulikana kuwa mkoa tajiri zaidi nchini Iraq. 

Jibu la pili ni kuwa, matukio ya juzi huko Basra khususan kuchomwa jengo la ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanaashiria kuwepo njama  ambazo si tu kuwa zinatekelezwa mkoani humo pekee bali katika pembe nyingine za Iraq. Kwa kawaida maandamano yayanayofanywa na  wananchi kulalamikia matatizo yanayowakabili si sababu ya  kushambuliwa na kuchomwa ubalozi mdogo wa nchi nyingine. Hata kama udhaifu wa askari usalama wa Iraq katika kuulinda ubalozi mdogo wa Iran hauwezi kufumbiwa macho lakini hakuna shaka kwamba kitendo hicho kimefanywa na watu ambao katika miezi ya karibuni wamekuwa wakifuatilia stratejia ya kuibua hitilafu kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.

Ubalozi mdogo wa Iran ukichomwa moto mkoani Basra, Iraq

Dalili nyingine inayothibisha kuwa kile kinachojiri huko Basra ni njama za nchi ajinabi zinazotekelezwa na vibaraka wa ndani ni hii kuwa makao makuu ya wapiganaji wa al Hashdu- Shaabi huko Basra yamechomwa moto. Hii ni katika hali ambayo kikosi cha al Hashdu- Shaabi kiliasisiwa na wananchi wa kusini mwa Iraq; huku kikosi hicho kikiwa na uungaji mkono mkubwa wa kijamii na vile vile mashahidi wake wengi wakitokea katika mkoa wa Basra.

Viongozi wa wafanya maandamano huko Basra pia wametangaza kuwa kuchomwa moto vituo vya kisiasa na ofisi za makundi ya muqawama ni kazi ya vibaraka kutoka nje  na wala hakuhusiani na wafanya maandamano.   

Machafuko ya basra yanaweza kuwa na matokeo hatari. Hata kama viongozi wa Iran na Iraq wamelaani matukio hayo ya Basra na kusisitiza kuchukuliwa hatua kali wahusika wa matukio hayo ya kusikitisha lakini wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imetoa taarifa na kukitaja kitendo cha kuchomwa ubalozi mdogo wa Iran mkoani humo kuwa sababu itakayoathiri maslahi ya Iraq na uhusiano kati yake na nchi nyingine za dunia (Iran). 

Athari nyingine muhimu ya matukio ya Basra ni namna yatakavyoathiri hali ya kisiasa na kiusalama ya Iraq. Katika hali ambayo makundi ya kisiasa ya nchi hiyo yanahitilafiana pakubwa kuhusu uundaji wa serikali; matukio hayo yote yanaweza kuzidisha hitilafu za ndani. Ni karibuni tu ambapo Iraq ilifanikiwa kujinasua katika hali ya mchafukoge iliyosababishwa na ugaidi wa kundi la Daesh. Matukio yanayojiri mkoani Basra yanaweza kwa mara nyingine tena kuitumbukiza nchi hiyo katika duru ya machafuko ya kijamii. 

Kuhusiana na jambo hilo, Sayyid Ammar al-Hakim Mkuu wa mrengo wa Hekima ya Kitaifa wa Iraq amebainisha wasiwasi wake kuhusu matukio ya karibuni huko Basra na kulaani kushambuliwa ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo. Aidha amesema kuitumbukiza nchi katika dimbwi hatari ni moja ya taathira muhimu na mbaya zaidi za machafuko hayo.  

Sayyid Ammar al Hakim
Maoni