Sep 09, 2018 07:33 UTC
  • Russia: Magaidi, White Helmets wakutana kupanga igizo la shambulizi la kemikali Idlib

Russia imesema magenge ya kigaidi na kundi eti la 'kutoa misaada' la White Helmets linaloungwa mkono na Wamagharibi yamekutana kaskazini magharibi mwa mkoa wa Idlib, kwa shabaha ya kuratibu igizo la hujuma ya kemikali nchini Syria ili kuielekezea kidole cha lawama serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema Moscow ina ithibati inayoonesha kuwa makundi ya kigaidi likiwemo la Jabhatu Nusra yalikutana na White Helmets Jumapili kupanga senario za mwisho za igizo la mashambulizi ya kemikali yatakayolenga miji ya Jisr ash-Shugur, Serakab, Taftanaz na Sarmin.

Njama hizo zinafanyika wakati huu ambapo Jeshi la Syria linajiandaa kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi yenye lengo la kuukomboa mkoa wa Idlib toka mikononi mwa magaidi.

Mkoa wa Idlib, ngome ya mwisho ya makundi ya kigaidi Syria

Hapo awali, Bashar Jaafari, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa alisema tayari serikali ya Damascus imelikabidhi Baraza la Usalama la umoja huo ushahidi kuhusu njama hizo za hujuma ya kemikali mkoani Idlib.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimekuwa zikiituhumu serikali ya Damascus kuwa imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake katika maeneo kama Khan Shaykhun na Ghouta Mashariki, na zimeshambulia vituo vya serikali ya nchi hiyo kwa kutegemea madai hayo bandia.

Tags

Maoni